SOMO: UNDANI WA MAOMBI (6) - MCHUNGAJI MADUMLA

Muumini katika maombi ©beliefnet 

Na Mchungaji Gasper Madumla

Kusoma sehemu iliyopita Bonyeza Hapa

(II) MAOMBI YA SIFA NA KUABUDU.

Bwana Yesu asifiwe…

Sifa na kuabudu ni mojawapo ya aina ya maombi ambapo mwombaji hutumia muda wake kusifu na kuabudu jina la Bwana katika uzuri na utakatifu kwa msaada wa Roho mtakatifu. Ikumbukwe kwamba sifa na kuabudu ni sehemu ya ibada.

Tena MUNGU hupendezwa na ibada ya namna hii ikiwa inatoka rohoni na kweli,maana biblia inasema Yeye huketi juu ya sifa;“Na Wewe U Mtakatifu,Uketiye juu ya sifa za Israeli.” Zab.22:3. Hivyo basi, sifa na kuabudu ni sehemu ya maombi kwa sababu kwa njia ya kusifu na kuabudu tunazungumza na Mungu labda waweza kusema kivipi? Ni hivi;

Tunaposifu na kuabudu katika roho na kweli iwe ni kwa njia ya kuimba au kunena sifa za Bwana,tunakuwa tukiwasiliana kwa ukaribu na Mungu wetu na mawasiliano ya namna hii yana nguvu ya ajabu ambapo BWANA MUNGU hushuka na kukutana na mahitaji yetu,mara nyingine hata tusipoomba matakwa yetu,Yeye huweka majibu. Hili nikuambialo hapa ni kweli na amin,jaribu kufanya hivyo kisha utaona milango ya mambo yako ikifunguka.

Si wengi wenye kuijua siri hii kwamba sifa na kuabudu ni sehemu ya maombi yenye nguvu sana. Kwa maana kuna kipindi hatuitaji kuomba~omba mambo yetu binafsi yaani isiwe kila siku uombapo, uombe “Baba naomba…” “Baba naomba…” bali kuna kipindi yatupasa kumsifu na kumuabudu Bwana katika Roho na kweli tu.

Bwana hutushindia vita na watesi wetu pale tunapokaza kumsifu Yeye katika Roho na kweli. Fikiria ; upo katika vita kali,labda adui yako amekuinukia kiasi kwamba umekosa msaada kwa ndugu zako hata rafiki zako wamekutenga, lakini ukaanza kumgeukia Mungu huku ukimuinua na kumtukuza ukisema;

“Wewe ni Mungu,Bwana wa vita,Mungu mzuri,mwenye nguvu ninakuabudu…. hata kwa hili ninalopitia sasa,bado wanipenda ninakuabudu Eeh Bwana Yesu,pokea sifa na utukufu maana wastahili….N.K” Je katika sifa zote hizi, BWANA hatakufanyia mlango wa kutokea katika hilo jaribu?

Jibu ni jepesi kabisa, ni Kweli Bwana atakupigania tu,kwa maana ulimuabudu katika roho na kweli. Labda nikuoneshe hili kibiblia, tunajua habari za wana wa Yuda chini ya utawala wa Yehoshafati kipindi ambacho waliinukiwa na mataifa matatu yenye nguvu. Mataifa hayo yalikuwa wana wa Moabu,wana wa Amoni na pamoja nao baadhi ya Wameuni(Waamoni). Watu hawa walikuja kupigana na watu wa Yuda chini ya utawala wake Yehoshafati.

Akini Yehoshafati,baada ya kuutafuta uso wa Mungu kisha wakaenda vitani,panapo majira ya vita,Yehoshafati akawaweka watu watakaomwimbia BWANA mbele ya jeshi lake. Kumbuka; akina Yehoshafati hawakuwa na uwezo wa kupigana na matifa hayo matatu,bali wao walimtegemea Bwana katika sifa na kuabudu huku wakisonga mbele za maadui zao ambao hao maadui walikuwa kwanza ni wengi pili walikuwa na silaha za kivita. Imeandikwa;

“ Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele.Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa.” 2 Mambo ya nyakati 20:21-22

Tazama hapo kwa makini; Hawa wakina Yuda ( Yehoshafati) walipoanza kuimba na kusifu,Bwana akaingilia vita hiyo naye Bwana akwapigania wakati akina Yuda wao wanaendelea tu kusonga mbele wakisifu na kumwimbia Bwana. Biblia inasema Bwana akaweka “waviziao” yaani watesi wakapigana wao kwa wao,ni kama vile walichanganyikiwa. Sijui kama unanielewa vizuri!

Si jambo jepesi hili,lakini inawezekana. Kumbe,vita si yetu bali ni ya Bwana,kwa maana Yeye Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki ( 1 Samweli 17:47 ) Lakini ni pale ambapo tunapokuwa tumejitoa kidhati kwa Bwana,naye Bwana hupigana mwenyewe.

Tatizo ulilonalo wewe mpendwa hutaki kujitoa kwa dhati kwa ajili ya BWANA ndio maana unatumia nguvu kubwa sana ya kupigana na maadui zako kwa sababu Bwana anakuwa hajausishwa. Akina Yehoshafati wasingeliweza kuwapiga maadui zao kama BWANA MUNGU asingehusishwa. Waweza kuniuliza Mungu alihusishwaje? Ni hivi;

Watu hawa kwanza waliomba,pili~Wakamsifu na kumuimbia Bwana Mungu katika uzuri wa utakatifu. Bwana akashuka na kuwashindia. Nikuulize swali moja; Je ni kweli katika ratiba zako,unatenga muda mzuri wa kumsifu Bwana na kumuabudu ? Kama la! Basi anza leo,hujachelewa.

Hata leo tunapitia vita nyingi sana,lakini ishu ni namna gani tunamtanguliza Bwana Mungu. Nahitaji kuomba na wewe kwa kile unachopitia,nipigie kwa +255 655 11 11 49.

ITAENDELEA…

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.