KANISA LA UFUFUO NA UZIMA LAKANUSHA TAARIFA ZA KUFUTIWA USAJILI NCHINI

Askofu mkuu wa kanisa la Ufufuo na Uzima Duniani Dkt Josephat Gwajima

Baada ya kuwepo ama kuzagaa taarifa za kufutiwa usajili wa kanisa la Glory of Christ Church International almaarufu kama Ufufuo na Uzima katika mitandao ya kijamii hususani Facebook, kanisa hilo limekanusha uvumi huo kupitia msemaji wao ambaye ndiye mkurugenzi wa kitengo cha habari na mawasiliano wa kanisa hilo mchungaji David Mgongolwa. kama inavyosomeka chini..
Aidha kusambaa kwa uvumi huo kunatokana na kukamatwa kwa muda kwa mahojiano na jeshi la polisi kanda maalumu ya Dar es salaam mapema hapo juzi kwa Askofu Josephat Gwajima aliyekuwa akirudi nchini akitokea nchini Japan ikiwa takribani mwezi tangu kuwepo kwa taarifa ya kutafutwa na jeshi hilo kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi, sambamba na taarifa za serikali kuzifutia usajili taasisi zaidi ya 500 nchini ambazo hata hivyo hazijawekwa bayana bado kwa wananchi.

Aidha tukio zima la kuhojiwa kwa askofu Gwajima limeandikwa na mtandao wa Mpekuzihuru kama taarifa nzima inavyojieleza hapo chini

Hatimaye Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye amekuwa akitafutwa na Jeshi la Polisi kwa siku kadhaa alikamatwa jana katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) alipowasili akitokea Japan.
Baada ya Askofu Gwajima kukamatwa na Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa JNIA alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.

Akizungumzia kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi Uwanja wa JNIA, Martin Otieno alisema askofu huyo aliwasili saa 2.45 asubuhi akitokea Japan kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.Otieno alisema mara baada ya kukamatwa alipelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.


“Ni kweli tulimkamata Askofu Gwajima hapa uwanja wa ndege wa JNIA baada ya kuwasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya na tulipomuhoji alidai kuwa alikuwa nchini Japan,” alisema Otieno. Mwanasheria wake Peter Kibatala alisema Gwajima alifika Kituo Kikuu cha Polisi saa 4.45 asubuhi kwa mahojiano mafupi na aliruhusiwa kuondoka baada ya kujidhamini yeye mwenyewe.

“Askofu Gwajima amehojiwa leo (jana) na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu na amejidhamini yeye mwenyewe, ameruhusiwa kuondoka hivyo tunasubiri chochote kitakachoendelea,” alisema Kibatala bila kueleza mahojiano yalivyokuwa. Askofu Gwajima alikuwa anatafutwa na polisi tangu mwezi uliopita baada ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya kijamii unaodhaniwa una sauti yake akipendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kufikishwa mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo sasa Rais John Magufuli anayashughulikia kwa mtindo wa kutumbua majipu.

Katika mkanda huo, sauti hiyo inadai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Rais Magufuli asipewe uongozi wa chama hicho kwa sasa kama ilivyo utaratibu wa chama hicho na kwamba hilo likifanyika basi Rais abadili katiba ili mstaafu huyo aweze kufikishwa kortini. Tangu ulipotolewa mkanda huo, makachero wa polisi wamekuwa wakipiga kambi nyumbani kwa Askofu Gwajima kwa lengo la kumkamata lakini hawakumpata.


Baadaye ilikuja kufahamika kwamba askofu huyo alikuwa amekwenda nje ya nchi lakini haikujulikana ni nchi gani. Hata hivyo, baada ya kutafutwa na polisi, Gwajima kupitia wakili wake Kibatala alisema atakaporejea nchini atakwenda moja kwa moja polisi kwa ajili ya mahojiano.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amekuwa akisisitiza kwamba jeshi litaendelea kumtafuta askofu huyo kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa, Interpol.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.