SOMO: UNDANI WA MAOMBI - (8 & 9) - MCHUNGAJI GASPER MADUMLAKusoma sehemu iliyopita bonyeza Hapa

(IV) MAOMBI YA KUMSIHI MUNGU NA KUMUULIZA.

Bwana Yesu asifiwe…

Neno “ kusihi” linawakilisha uombaji wa upole wenye kuonesha huruma ya mwombaji. Mfano mtu akikuambia “ninakusihi usimuadhibu...” sentesi hii,ni sawa na kusema “ninakuomba kwa huruma yote,usimuadhibu”. Tunapomsihi BWANA MUNGU katika maombi yetu,ni sawa na kushuka mpaka chini tukiomba kwa huruma na unyenyekevu,kwa hiyo utagundua kwamba ni aina ya maombi ya utulivu.

Na ikiwa ni hivyo basi utulivu wa moyoni utiisha na mwili pia,ndio maana mwili ukitiishwa utaona matokeo,utaanza kupiga magoti,waweza hata kulala kifudi fudi (ishara ya kushuka zaidi hata mavumbini).Tazama,mara nyingi maombi ya kumsihi Mungu huambatana na kushuka zaidi chini ya Mungu. Tuangalie biblia inasemaje;

“Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake;” Luka 8:41 tazama tena hapa;

“Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.” Mathayo 18:29

Musa naye alimsihi Bwana Mungu pale ambapo watu wake walipofanya uovu;“Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa.” Hesabu 14:19. Hivyo basi neno hili “kusihi” mara nyingine hutumika katika maombi ya toba. Mfano; “ninakusihi eeh Bwana, unisamehe”

Maombi ya namna hii ni muhimu sana,kwa maana si wengi wenye kuyafanya. Watu wengi wana maombi ya kushauti na sio ya upole kwa kushuka chini ili Bwana apande.

Watu wengine wanafikiri kwamba wasipoomba kwa kushauti yani kwa sauti kubwa Mungu awasikii,wamesahau kwamba Mungu huangalia moyo.(Sisemi usitoe sauti kila uombapo,bali kuna kipindi fulani yakupasa uombe katika hali ya utulivu wewe na Bwana Mungu wako)

Tuangalie maombi ya kumuuliza Mungu,maana yake nini haswa? Je ni kweli mwanadamu aweza kumuuliza Mungu? Tunafahamu kwamba neno “ kuuliza” huja baada ya kuwepo na swali au kuwepo na hali ya sintofahamu.

Ni ukweli kabisa kwamba sisi hatustahili kujifananisha na Mungu,kwa maana Yeye ni mkuu sana na hakuna kama Yeye. Katika hali ya kawaida huwezi kumuuliza mtu aliye juu yako eti kwa sababu hajakutimizia haja yako. Mfano je unaweza kumuuliza boss wako eti kwa nini umechelewa ofisini?

Yule anayepaswa kuulizwa ni yule aliyepo chini ya..,boss wako anapaswa kukuuliza wewe kwa swali kama hilo. Lakini hali hii inawezekana tu pale ambapo utakuwa na ushirika mkubwa sana na boss wako,hapo waweza ukamuuliza kwa upendo kabisa naye atakujibu vizuri tu katika upendo. Alikadhalika kwa Mungu ni vivyo hivyo.

Tunapokuwa na ushirika mzuri na Mungu wetu,tunaweza kumuuliza baadhi ya mambo yanayotutokea tusiyoyatarajia. Lakini ni lazima uwe na mausiano mazuri na Bwana Mungu wako,la sivyo huwezi ukamuuliza,chukulia huo mfano wa boss na mfanyakazi wake. Tuangalie biblia inasemje kuhusu hili,tunasoma;

“ Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.” 2 Samweli 21:1

Tunamuona Daudi akiutafuta uso wa Bwana,alipoutafuta Bwana akamjibu… Hapa ninajifunza jambo moja kwamba,Daudi alimuuliza Bwana kwa nini njaa hii ya miaka mitatu mfululizo? Daudi hakuanza kupambana na hali hiyo ya ukame bali alianza na kumuuliza Bwana. Wewe pia waweza ukamuuliza Bwana Mungu katika hali unayopitia.

Lakini ukumbuke kwamba ni lazima uwe mwenye haki,uwe na kibali ndiposa upokee majibu ya maswali yako. Kwa lugha nyepesi Daudi alipata kibali machoni pa Bwana.

Emu fikiria, unpokwenda kumuuliza mtu wa kawaida pale usipopata kibali,je utajibiwa? Ni kama vile unaanza kumuuliza “ Kwa nini sina pesa hivi?” Naye atakujibu “ kamuulize babako” au kama ndio ukimkuta mstaarabu aweza kukujibu“Sa mi nikusaidieje?,niko bize bhana…” N.K Umeona!!

Majibu ya mkato mkato yamekuja kwa sababu huna mahusiano mazuri wala huna kibali. Lakini laiti kama utakuwa na kibali,basi chochote utakachoulizwa kitakuwa na majibu yake yanayostahili.
Bwana Yesu asifiwe…

Hii ni aina ya tano ya maombi ( kwa mujibu wa mpangilio wangu). Unaposikia neno hili “maombi ya vita” unapata picha gani? Au unaelewa nini? Msamiati mkubwa upo katika neno “vita” Hivyo,leo hatuna budi kujua vita hii ni vita gani,na kwa nini kuna maombi ya vita.

Tafsiri nyepesi ya neno “vita” lina maana ya mapigano/mashindano/mapambano baina ya pande pili. Na katika vita kuna mawili tu,kushinda au kushindwa wala sijawahi kuona kutoka suluhu katika vita,sijui kama kuna kutoka suluhu bali ni kupiga au kupigwa ndilo nilijualo.

Tabia ya vita,ni lazima kuwe na ugomvi/uchokozi au kuwe na upinzani usiowezekana kutatuliwa mpaka kupigana,mshindi ndiye atakaye muongoza mnyonge wake. Vita yoyote ile ni lazima itumie silaha,wapiganaji na uwanja wa kupigana.

Hayo matatu ni muhimu sana katika kila aina ya vita. Lakini ikumbukwe hili; kiongozi wa vita ni muhimu sana na lazima awepo katika kila aina ya vita. Lakini mpaka vita kupiganwa ujue kuna sababu,la hakuna vita.

Katika uzoefu wangu mdogo,sijawahi kuona mpiganaji ndani ya vita anayekata tamaa. Huwa sikuzote wapiganaji hawakati tamaa wakiamini watashinda. Kule kuamini ushindi ndiko kunakowapea nguvu ya kusonga mbele kupigana.

Labda tujikumbushe yale ya kitambo yaliyowahi kutokea katika nchi yetu katika utawala wake Mwl. pale alipotangaza kumpiga Iddi Amin dada,alisema~ uwezo,nia na nguvu tunazo za kumpiga Iddi Amini. Hii inatuonesha kwamba mpiganaji hujiamini kwamba atashinda kumpiga mpinzani wake. Kwa maelezo hayo,sasa tujiulize swali hili;

Sasa,kwa nini sisi wakristo tunaomba maombi ya vita?,je ni vita gani? Jibu lake ni jepesi tu,tunafanya maombi ya vita kwa sababu tunayo vita dhidi ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kumbe,kuna falme ya giza ya yule mwovu twapasa kuipiga,kuwapiga tena wakuu wa giza hili(Wachawi,waganga,majini n.k),tena tuwapige majeshi ya mapepo katika ulimwengu wa roho.(Waefeso 6:12)

Ukitambua ya kwamba,shetani yupo,naye yupo akishindana nasi basi ni lazima utangangana kujua namna ya kupambana naye katika ulimwengu wa roho. Kile ninachotaka ujue kwamba maisha yako si salama kwa maana yana vita, tena yeyote aliyeokoka ametangaza vita dhidi ya falme na mamlaka,dhidi ya mapepo. Hivyo basi huna budi kupigana!

Rejea maelezo ya vita ya hapo juu, kisha linganisha sasa;sisi wakristo tunayo vita na jeshi la shetani. Ugomvi wetu mkubwa ni kwamba yeye shetani anataka kutuangusha tumtumikie lakini sisi hatupo tayari kwa maana wakutumikiwa ni mmoja tu naye ni JEHOVA pekee.

Uwanja wetu wa mapigano ni katika ulimwengu wa roho,huku tukitumia silaha za rohoni katika maombi. Nia tunayo,nguvu tunazo na uwezo pia tunao wa kumpinga naye atatukimbia tu. Tumepewa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge,tunasoma;

“Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.” Luka 10:19

Sasa,utagundua kwamba kupigana kwetu si juu ya damu na nyama bali katika ulimwengu wa roho. Tunapigana na falme ya giza na majeshi yake. Tunazo silaha za kutosha kumpiga shetani katika maisha yetu katika jina la Yesu Kristo. Lakini sharti tuwe kwa Bwana,kwa maana Yeye Bwana ndie apiganaye.

Maombi ya vita ni maombi kupambana na kila aina ya nguvu ya giza katika ulimwengu wa roho,maombi haya ujulikana pia kwa jina la “maombi ya kuvunja na kuharibu utawala wa kipepo“. Pale uonapo mambo hayaendi,pale uonapo roho ya magonjwa imeachiliwa kwako hata katika familia,ukoo N.K

pale uonapo roho za mauti ndani yako,N.K Hapo ushtuke ukijua kwamba huyo ni adui,amerusha mishale,nawe usikae kimya,amka na kupambana naye kwa njia ya maombi katika ulimwengu wa roho.

Wapo watu wasiojua undani wa maombi haya kiasi kwamba warushiwapo mishale na yule muovu,wao hudhania ni Mungu kawapiga kumbe sivyo,ni shetani tu mwenye kuvuruga maisha yao. Si kila gumu linaachiliwa na Mungu,mengi hutoka kwa shetani akikukinga usije ukafanikiwa. Leo,huna budi kumshughulikia adui yako katika maombi ya vita kwa mamlaka na nguvu ya jina la Yesu pekee na damu yake.

Siku moja,wakati naongea na mtu mmoja aliyekuwa akivamiwa na mishale ya kipepo. Aliniambia akiona wanakuja usiku yeye uamka na kumwaga maji ya baraka kisha umwaga hayo maji kwenye kona kona ya chumba chake akiamini kwamba hayo maji ya baraka yatamkinga na uvamizi wa kipepo,kisha hurudi kulala.

Sasa angalia matokeo yake;

mapepo yalikuwa yakiingia kama kawaida,na kumtesa vile wapendavyo wao. Yale maji hayakuwa na msaada wowote ule. Lakini emu jiulize sasa,kwamba shetani utamzuia kwa maji ya baraka? Kwa hiyo ni kama vile alikuwa akimbariki shetani azidi kuingia!!! Huu ni utoto kwa kweli.

Angalia shetani alivyopofusha akili za wengi,utakuta mtu anatumia maji kama ulinzi badala la jina la Yesu Kristo. Alufu naye shetani hujifanya kama vile anatoka ili yule anayetumia maji kama ulinzi wake,aamini na kumuacha Yesu mwenye nguvu. Ifike wakati sasa tutambue ya kwamba hatuwezi kulindwa na chochote isipokuwa jina la Yesu tu.

Maombi ya vita ni muhimu sana kufanywa kila wakati ili uweze kushinda vita unayopitia….Kumbe ishu sio kuomba tu,bali ishu ni kuwa mwenye haki kwanza ili kuomba kwako kusizuiliwe…. Ukiwa umeguswa na ujumbe huu,na unahitaji maombi nipigie sasa kwa +255 655 11 11 49.

ITAENDELEA….

Mchungaji G.Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.