SOMO: VIFUNIKO VYA KICHAWI - ASKOFU JOSEPHAT GWAJIMAVIFUNIKO VYA KICHAWI
Mungu hufanya kazi kupitia watu na ili Mungu afanye kazi lazima aingie ndani ya mtu ndipo aweze kufanya kazi vivyo hivyo na shetani hufanya kazi kupitia watumishi wake ambao ni wachawi, waganga, wasoma nyota, wapiga ramli, wasihiri nk na bila hao hawezi kufanya kazi hapa duniani. Usipohubiri Injili isiyowagusa watendakazi sio wa shetani unakuwa unakosea sababu Yesu alikuja kuwaweka watu huru kutoka kwenye utawala wa giza wa shetani.


Uumbaji wa Binadamu umeumbwa na Mungu ili afaulu, asipofauli ni Mungu ameshindwa. Dunia imeumbwa kwa namna kwamba kufanikiwa ni rahisi kuliko kushindwa! mfano ndege ameumbwa na ndani yake amewekewa uwezo wa kupaa kwenda sehemu ya mbali ambapo wewe unatumia fedha nyingi kuifikia, Samaki ameumbwa na Mungu na amepewa uwezo wa kukaa ndani ya maji ambamo wewe ukiingia lazima uzibe pua, isingewezekana basi wa kufeli wa kwanza ni Mungu na sio Samaki. Mwanadamu ameumbwa kutembea juu ya uso wa dunia ili kufaulu, Mungu anapotengeneza kitu amekitengeneza ili kifaulu kwahiyo kama ukishindwa kufaulu lazima ujiulize kwanini haufaulu. Mfano mzuri mtoto mdogo anapozaliwa tu anajua kunyonya ziwa la mama na sio kupuliza. kwanini hatafuni au hapulizi ni kwasababu hajafundishwa bali amepewa uwezo wa kufaulu kunyonya. Kila mtu amepewa uwezo wa kufaulu kwenye eneo lake tangu akiwa tumboni mwa mama yake wengine kwenye kuongea, kwenye biashara, kwenye kazi, kwenye kufundisha, kwenye kuhubiri, kwenye uongozi n.k Kila mtu ameumbwa ili afanikiwe.

Warumi 8:29 “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”

Yeremia 1:5 “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana. Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako;
angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.”

Yeremia alipewa ufaulu kwenye eneo la Unabii lakini Mungu alipoongea naye yeye alifhamu sawa anatakiwa awe nabii lakini alidhani yeye bado ni mtoto hivyo hawezi kuwa nabii mpaka awe mtu mzima lakini Mungu alimhakikishia kwamba aliumbwa awe nabii tangu tumboni mwa mama yake. Kumbe kila mtu amepewa uwezo wa kufanikiwa tangu tumboni mwa mama yake (tangu asili) Unapoona mtu hawezi kufanikiwa hapo ndipo tunaanza kugalia kuna vifuniko vya kichawi.

Ezekieli 28:13 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako”

Haya maandiko yanamwelezea shetani ambaye kabla hajawa shetani alikuwa malaika mzuri tu aliyezungukwa na madini ya aina hiyo na alikuwa malaika wa ngazi ya kerubi, alikuwa akiitwa kerubi mwenye kutiwa mafuta (mwenye kutiwa mafuta maana yake “amewezeshwa”) afunikaye. Alipewa uwezo wa kufunika. Mungu alipokuwa akitaka kwenda mahali shetani ndiye aliyekuwa akitangulia kufunika mahali pale halafu Mungu anakuja. Kerubi alikuwa akifika mahali alikuwa anapafunika sura sawasawa na kusudi la siku hiyo na baadaye kusudi likiisha anaondoka. Tunaona kumbe kazi ya kerubi huyu alikuwa anapamba kwa maana nyingine eneo fulani,sasa hivi bado ni kerubi anaoule uwezo na anaweza kufunika sura yako ukakuwa tofauti kabisa.

Ezekiel 41: 18 “kulipambwa kwa makerubi na mitende; mtende mmoja kati ya kerubi na kerubi, na kila kerubi lilikuwa na nyuso mbili; basi palikuwa na uso wa mwanadamu kuelekea mtende mmoja, na uso wa mwana-simba kuelekea mtende wa pili; ndivyo vilivyofanyika katika nyumba nzima pande zote.”

Unaweza ukajiuliza kwanini Mungu hakumnyanganya shetani ule uwezo wake, ni kwasababu Mungu akikupa amekupa iwe umekitumia vibaya au vizuri utakuja kukutana naye kwa wakati wake alioupanga. Unaona tatizo ni shetani anauwezo wa kumfunika mtu kwenye, biashara, sura, elimu, kazi, ndoa asionekane.

Wachawi wanauwezo wa kumfunika mtu, wewe unaweza ukawa unatafutwa na mtu fulani akuinue lakini huonekani kwasababu umefunikwa. Wachawi na waganga wamepewa uwezo huo na shetani ambapo mtu anaweza kuwaendea ili amfunike mtu mwenye wivu nayeye asionekane kwenye kupata kazi, kufanya biashara, uso wa mvuto, unakuta mtu anajaribu kujipamba na kuvaa vizuri lakini akitoka haonekani mbele ya watu kwasababu amefunikwa na wakala wa shetani. Tatizo sio kuvaa vizuri, sio kujipodoa, sio nguvu za Mungu, sio kupendwa na Boss tatizo ni kuonekana vifuniko ya shetani.

Yaobo1: 17 “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”

Kila mtu ni mzuri kwa namna yake hatakama ana jicho moja, ana mkono mmoja, ni mfupi au mwembaba, ni mnene au mrefu kila mtu ameumbwa na Mungu kwa namna ya ajabu umefanana na Mungu. Kilamtu ni mrembo kwa umri wake, bibi wa miaka themanini ni mrembo kwa mzee wa miaka themanini, kila mtu mwenye miaka thelathini ni mrembo na mtanashati wa miaka thelathini usijipunguze au kujiongeza kucha sababu Mungu anakupenda na wewe ni wathamani kubwa sana machoni pa Mungu.

Kutoka 25: 19 “Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema.”

Ezekieli 28:16 “Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.”

Ezekieli 10:3 “Basi, makerubi walisimama upande wa kuume wa nyumba, hapo alipoingia mtu yule; nalo wingu likaujaza ua wa ndani. Utukufu wa Bwana ukapaa kutoka kwa kerubi yule, ukasimama juu ya kizingiti cha nyumba; nayo nyumba ikajazwa na lile wingu, na ua ulikuwa umejaa mwangaza wa utukufu wa Bwana.”

Ukiri:-
“Kwa jina la Yesu kuanzia leo ninakataa kufunikwa kichawi kwa damu ya Yesu”

Kwa kawaida shetani akishindwa kukufunika huwa anahamishia kiti cha enzi nyumbani kwako ili ashindane na wewe. Shetani anapoona wewe kuna mahali ambapo unaweza kupenya huwa anahamia kwako, kwenye afya, kwenye Elimu, kwenye familia.

Kerubi anaweza kukaa akawa mlinzi, shetani ni kerubi kwahiyo kila anachoweza kufanya kerubi mtakatifu basi na yeye anaweza kufanya.

Mwanzo 3:24 “Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima”

Mungu alimweka kerubi ili wasiweze kupita hiyo njia sababu alijua kutembea kwenye ile njia kuelekea kwenye mti uzima wanaweza lakini lazima kerubi awepo ili kuwazuia wasipite. Kwenye maisha yako unajua kabisa ajira ipo pale, biashara ipo pale na unaiona njia ya kufanikiwa ipo wazi lakini unapambana ili ufanikiwe kupita inashindikana kwasababu kerubi huyu analinda usipite.

Tunaona kwenye Biblia mtu mmoja alikuwa anaelekea Yeriko na njiani akakuta wanyanganyi wakampiga Biblia inasema ‘wakamwacha nusu mfu’, alipopita mlawi(mchungaji) alipomwangalia akapita pembeni baadaye akapita kuhani (mchungaji) naye akamwacha na baadaye akapita msamaria mwema akamchukua na kumpeleka akatibiwa na kulipa gharama zote. Leo yupo msamaria mwema Yesu kristo amepita ili akuokoe dhidi ya kerubi afunikaye na kukupelekka kwenye mafanikio yako.

SIFA ZA KERUBI AFUNIKAYE

1. Wana nyuso zaidi ya moja
Ezekieli 10:21 “Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne; na mifano ya mikono ya mwanadamu ilikuwa chini ya mabawa yao.”

2. .Ana macho pande zote.
Shetani anasifa ya kuwa na macho kila mahali

3. Wana mabawa manne.

AINA ZA VIFUNIKO VYA KERUBI HUYU AFUNIKEYE.

1. Kifuniko cha tabia.

Mithali 17: 8 “Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho; Kila kigeukapo hufanikiwa.”

Yakobo 3:15 “Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani.”

Mungu amempa kila mtu kipawa ili kusudi kimsaidie kufanikiwa. Shetani anaweza kukufunika kwa tabia mbaya usifanikiwe.

Rahabu alikwua kahaba lakini kwenye Ukoo wa uzao wa Yesu yumo mmoja wao. Wana waIsraeli walikwenda kuichunguza walipofika Yeriko wakakutana na huyu Rahabu ambaye aliwasaidia kuwahifadhi wakaupeleleza mji ule baadaye wakaja wakashinda na kuuteka, Unaona Rahabu alikuwa amefunikwa na tabia ya kikahaba sababu shetani alijua kupitia yeye Yesu atapatikana, Mungu aliwaambia wana wa Israeli wamwache yule Rahabu sababu amampango nayeye.

Wewe sio Yule ambaye watu wanasema, wewe sio yule ambaye adui zako wanasema upo hivyo. Mungu anampango na wewe usiogope, usiangalie maisha uliyopitia na unayopita sababu shetani amekujaza vifuniko lakini hakuna kitu cha kumzuia Mungu aache kukuokoa Simama ukauone wokovu wa Mungu maana wale wamisri mnaowaona leo hamtawaona tena, utawatafuta waliofanya vita juu yako hautawaona tena mana Mungu kwetu ni Mungu wa kuokoa na njia za kutoka mautini zina yeye.

Wamemjaza Rahabu vifuniko vya mbaya na mtaani wanamsema anatabia mbaya lakini alikuwa na kusudi la Mungu na ule haukuwa mwisho wake. Kwahiyo wanaeza kukujaza na tabia mbaya sababu wanachungulia mbele utangaa kama nyota ya asubuhi lakini wale walioshindana na wewe utawatafuta na huta waona tena.

Kwahiyo kuna vifuniko vya tabia ambavyo unakuwa umefunikwa bila wewe kujua. Mfano Rahabu hakuzaliwa ili awe kahaba, amewekewa ukahaba ili ashindwe kutimiza kazi aliyopewa na Bwana, lakini hakuna kilichomzuia asitimize kazi ya Bwana hivyo basi nawewe usijilaumu na tabia uliyo nayo sababu umewekewa uwezo wa kushinda na utatimiza lakini kumbuka jambo moja.

Mithali 28:13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

2. Kifuniko cha udhaifu

Mashetani yote duniani yanauwezo wa kugeuka na kuwa ugonjwa na udhaifu. Mojawapo ya matukio kwenye mwili ni damu kusafiri kwenda kwenye mwili wote tokea kwenye moyo. Moyo kabla haujasafirisha damu unajipa wenyewe halafu unapeleka kwenye Ubongo, kwenye ini, kwenye na baadaye kwenye viungo vingine kwasababu damu ikiingia kwenye ubongo uwezo wako wa kupanga mipango unaongezeka, uwezo wako wa kufikiri unaongenezeka sasa wanajaribu kukuwekea magonjwa ili ule uwezo wako wa kufikiri usifanye kazi sawasawa, mashetani wanakawaida kwamba ukiamka asubuhi ujiskie kichwa kinauma, kifua kinauma, unapumua vibaya unapooza ili ushindwe kupanga mipango ya maana ya kufanikiwa wale wasiokupenda wanakuwekea mapepo kwenye mwili wako na kibaya zaidi wewe unadhania ni ugonjwa lakini sio ugonjwa ni kifungo cha afya.

Kuna watu wakiwa wazima wanapanga mipango ya maana lakini shetani amewafunika ili wawe dhaifu muda mrefu.

“Kiri”
“kwa jina la Yesu navunja kifungo cha afya dhidi yangu kwa jina la Yesu”

Luka 13:11 “Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.”

Ukiwa mgonjwa hata inapotokea kazi fulani wanasema yule ‘mgonjwa hawezi’, ukipata nafasi ya biashara wanasema ‘wewe si mgonjwa huwezi kufanya’ sababu umefunikwa kifuniko cha udhaifu usifanikiwe wanajua ukiwa mzima hatima yako ni kubwa sana hivyo wanakuzuia usiitimize.

Luka 5: 1 “Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe. Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.”

Mtu huyu alikuwa mhubiri tangu asili lakini alifunikwa na jeshi la mapepo akawekwa njiapanda kuzuia watu wasipite lakini Bwana Yesu alimwona na kuvuka kwenda kumfuata na kumfungua na baada ya kufunguliwa akaenda kutimiza kusudi lake kwenye miji Dekapoli 12.

3. Kifuniko cha akili.
Waefeso 4:18 ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao”
2 Wakorintho 4:4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu

4. Kifuniko cha umaskini.

Mwenye fedha akiwa na shida ya kujenga nyumba anaweza kutumia fedha yake akaitatua shida ya kujenga nyumba. Shetani akiona wewe ni hatari kule mbele uendako anakufunika kwa kifuniko cha umaskini ili ukwame njiani.

Palikuwa na mfalme aitwaye Daudi ambaye ni mwana wa Yese aliyetoka kwenye familia ya kimaskini, Nabii wa Mungu alifika kwenye familia yake akamwambia mzee Yese kesho aje kumpaka mwana mafuta mwanae mmoja ili awe Mfalme, kaka zake walikuwa wenye uwezo wa kivita walionekana ndio wenye mwonekano wa kifalme, Samweli alipokuwa akiangalia kaka zake daudi akamwona mmoja akadhania yeye ndiyelakini alipotaka kumwekea mafuta Mungu alikamkataza sababu hakuwa ndiye, Samweli alipoona hayo alimuuliza mzee Yese hawa ndio wanao wote? Mzee Yese akamwambia ndio ila kuna kamoja kapo lakini hakana mazoezi ya vita, ndipo Samweli akaamuru aletwe naye akaletwa akawekewa mafuta na Daudi akawashangaza sana Baba yake na ndugu zake kuwa yeye ndiye atakayekuwa Mfalme wa Israeli.

Cha kushangaza wale ambao hawakupakwa mafuta ndio waliokwenda kwenye vita, (mwenye kupakwa mafuta ndiye anayeshinda vita) vita kati ya Israeli na wafilist walikubaliana kila mmoja atoe mtu mmoja ambapo kule kwa wafilisti walimchagua Goriathi ili awe shujaa wao na kwaniaba ya Taifa na Israeli nao wakamchagua mtu wao kwaniaba ya Taifa lakini upande wa Israeli wakamtoa Daudi akaamua kumwendea Mfalme ili yeye apigane na Goriathi na kumwaga CV yake kwamba ‘siku moja alikuwa anachunga kondoo wa Baba yake akaja Dubu anakata kula kondoo akamkamata akamuua na siku nyingine akaja Simba akamrukia akamtawanya na huyu mifilisti aiyetahiriwa nitamfanya vivyo hivyo’ kwa maneno yale Mfalme akamruhusu aende.

Goriath alikuwa amezungukwa na watu wane waliomshikia silaha na Daudi yeye alikuwa peke yake akamwambia kichwa chako kitakuwa chakula cha mbwa kwasababu umeyatukana majeshi ya Bwana. Daudi akabeba mawe sita japo walikuwa watano. Daudi alianza na mkubwa wao Giliath (Ukitaka kuanza kupigana vita anza na kuwa yao) Goriathi alikuwa amejiziba uso wake kwa kinga lakini jiwe la Mpakwa mafuta llimpata na kumwangusha chini (Jiwe la mpakwa mafuta halikosi), na wale walipoona shujaa wao amekufa wakakimbia wote wana wa Israeli wakawakimbiza na kuwaangamiza wote. Tangu wakati ule Daudi akawa mkuu kutoka kwenye kifuniko cha umaskini na kudharauliwa.

2 Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”

2 Mambo ya Nyakati 1:12 “Basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.”

Mtu anayetaka kukufunika hunatuma mashetani kuja kukufunika uso wako ili usionekane. Mganga hufanya kazi baada ya kupelekewa mashtaka ya mtu anayetakiwa kumfungwa, kila mtu anao wasiompenda mpaka Mungu anaadui, yule mtu asiyekupenda huwa anaenda kwa mganga na kumwambia kuna mtu fulani mfunike uso wake au akili yake,na wewe bila kujua unafunikwa akili unafanya maamuzi mabaya, kama umeolewa unafunikwa kifuniko cha utasa ili usizae mtu atakayekuwa mwanasayansi, au Askofu, au Raisi, au Mfanya biashara mkubwa. Wanapozuia usizae sio kwamba hawakupendi bali wanazuia kilichombele yako kwamba utazaa mtu wa maana sana duniani, unakuwa ukitunga mimba unatunga mimba zilizoharibika, uso ukifunikwa unakuwa unachukiwa na watu bila ya sababu na wewe unashangaa, unafunikwa kinywa unakuwa unaongea mambo yasiyo na maana ambayo yanakuleea matatizo, akili inafunikwa unakuwa huwezi kuwaza mipango ya mafanikio.

Yule mtu unayeshindana naye siyo mchawi lakini anawaendea wachawi wanawatumia mashetani ambao huwatuma kwako kukufunika eneo unaloonekana ni linamafanikio litakufanikisha. Hakupendi kwasababu unaakili sana, unauwezo wa kufanya kazi vuzuri, unanyota ya kupendwa, unamikono iliyobarikiwa, wanakufunika usionekane.

Kumbuka shetani anaweza kutenda kazi kwa namba mbili akiwa ndani yako (unakuwa umepagawa) au nje yako kama:-

Zekaria 3:1 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye.”

Kifuniko sio kama kofia ni jini au pepo lililopewa damu ama udi ama ubani ambalo linatumwa kumwingia mtu usoni, kweye tumbo, kwenye akili, kwenye mkono, kwenye kifua bila yeye kujua. ameambia aingie kwake kwasababu kuna dalili njema ya maisha yake, na akishafunikwa matatizo ndiyo yanaanza sasa

“Kwa jina la Yesu vifuniko vya kichawi ninaviondoa kwa jina la Yesu, vifuniko vya biashara, vya kazi, vya safari, vya watoto, vya akili, vya mikono naviondoa kwa jina la Yesu nafungua moyo wangu, akili yangu, mikono yangu, tumbo langu, uso wangu enyi mashetani ondoka sasahivi funga virago kwa jina la Yesu”

Shetani ni kerubi afunikaye na huwa anawafunika watu wanaomwabudu ili waonekane japokuwa hawana sifa ya kuonekana kwenye sehemu mbalimbali, iwe ni serikalini, iwe kwenye biashara unakuta mtu hafai kuwa kwenye sehemu hiyo lakini yupo hapo na anafanikiwa na wale wanaostahili kuwepo hapo hawapo ni kwasababu amefunikwa na shetani ili aonekane anafaa.

Mathayo 4: 8 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia. Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.”

Wewe hapo ulipo hauhitaji nguvu bali ni kutumia jina la Yesu kwa mamlaka “katika jina la Yesu jini lililonifuka nakuamuru niache na uondoke kwa jina la Yesu, kama umempokea Yesu. umeingia kwenye Ufalme wa Mungu na wewe ni mwanafunzi wa Yesu unayo mamlaka juu ya pepo wachafu. Mtu yeyote aliyempokea Yesu moyoni mwake ndani yake nguvu juu ya mashetani hawa ambao ni vifuniko wanafunika watu. Kwahiyo unakuwa unaomba katika jina la Yesu ninaondoa vifuniko vya akili yangu kwa jina la Yesu, vifuniko vya akili, vifuniko vya biashara, vifuniko vya kila aina na ukishaomba hivyo utaanza kuota ndoto ya maisha yako ya baadaye na Mungu atakubariki.

Luka 9:1 “Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.”

Mathayo 10:1 “Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.”

Mashetani wapo wa vifuniko vya kila aina sehemu uliyobarikiwa, ukishafungua vifuniko hivyo utaanza kuona ulikuwa hupendwi na watu unaanza kupendwa, ulikuwa ukiomba kazi hupati lakini ukiomba unatafutwa sababu vifuniko vimeondolewa na unaanza kuonekana na kungaa. Unapokuwa umefunikwa wewe huwezi kujua lakini kunakuwa na mtiririko wa matukio ya balaa kwenye maisha yako mara kuibiwa, mara kutukanywa, mara kuugua, mara kuishi maisha ya umaskini, mara kukata tama, mara kujichukia, yote haya ni kwasababu ya vifuniko vya kichawi.

Shetani ni kerubi afunikaye na anatenda kazi kupitia wakala wake, simama kwa mamlaka ya Jina la Yesu kufungua vifuniko vya kichawi kwenye eneo la maisha yako na utakuwa huru na kufanikiwa kuwa jina la Yesu kristo Amen.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.