SOMO: KUWAELEWA MANABII WA AGANO JIPYA LA NEEMA - PASTOR CARLOS KIRIMBAIKUWAELEWA MANABII WA AGANO JIPYA LA NEEMA.

Ukiingia mtaani ukakutana na bidhaa feki moja ya vitu ambavyo utavigundua ni kwamba ile bidhaa feki inakaribiana sana na ile halisia na inahitaji mtu mwenye ufahamu sana na bidhaa halisia ilivyo kuweza kung'amua na kutambua bidhaa feki.

Katika zama zetu huduma feki nyingi mno zimeachiliwa na kama huna ufahamu wa ile halisia inatakiwa kuwaje ni rahisi sana kudanganyika na kudhani kuwa unapokea huduma halisia kumbe unapokea huduma feki na madhara yake ni makubwa sana kama ambavyo madhara ya kutumia bidhaa feki ilivyo kubwa.

Sio kila ajiitaye nabii ni nabii kweli na sio kila ajiitaye mtume ni mtume kweli wala muijilisti, mchungaji na mwalimu.

Kinachotuonyesha huduma halisi inafananaje ni maandiko na kama hujui huduma ilivyo kwa mujibu wa maandiko ni rahisi sana kudanganyika ukadhani unapokea toka kwa huduma halisi.

Moja ya uongo mkuu sana ambao unatumika kuwadanganya watu kuhusu huduma ya kinabii ni kwamba huduma ya kinabii katika Agano Jipya haina tofauti na ile ya Agano la Kale.

Kuna tofauti kubwa mno ya kiutendaji kati ya huduma ya nabii katika Agano Jipya na la Kale kama mchana na usiku.

Sababu na makusudi ya huduma hiyo kuwepo katika Agano Jipya sio sawa hata kidogo na sababu na kusudi la kuwepo kwake Agano la Kale.

Ingawaje sio sehemu ya post hii kuchambua kwa undani huduma ya kinabii ya Agano Jipya kuna kitu kimoja nataka nikiweke hapa ambacho miongoni mwa vingi kama hakipo sawa ni ishara wazi kuwa hiyo sio huduma halisi ya kinabii kwa vigezo vya Agano Jipya.

Kwanza Nabii wa Agano Jipya anamfunua Kristo na sio shetani na kazi zake.

Unabii wa Agano Jipya haukuonyeshi shetani anafanya nini bali unakuonyesha Yesu anafanya nini.

Msingi wa utendaji wa huduma ya kinabii katika Agano Jipya ni Neno la Mungu na unabii wao unatoka katika Maandiko.

Nabii anayo neema ya kutusaidia kuona jinsi ambavyo neno la Mungu ni halisi na linaweza likatumika leo kukabiliana na changamoto tunazokutana nazo.

Nabii wa Agano Jipya hajajikita sana katika kuyaelezea matukio yajayo bali kwenye kulizungumza Neno la Mungu kwa nguvu na uvuvio wa Roho Mtakatifu.

Nabii wa Agano Jipya amejikita sana katika kulisoma neno la Mungu ili awe na uwezo wa kuja lisema kinabii kwa udhihirisho wa nguvu na uvuvio wa Roho Mtakatifu.

Huduma ya Neno ya Nabii inaambatana na udhihirisho wa nguvu za Mungu, ishara na maajabu ya Mungu.

Ila jambo moja ni hakika kabisa, huduma ya nabii italisaidia kanisa kumfahamu sana Mwana wa Mungu na kulisaidia kanisa likue kufikia cheo cha kimo cha utimilifu cha Kristo.

“Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi. Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu. Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.” (UFU. 10:8-11 SUV).

Ili Mtume Yohana aweze kuwatolea unabii watu na taifa na lugha na wafalme aliamuriwa akile kitabu na hicho kitabu atakachokula kitakuwa kitamu kinywani mwake bali chungu tumboni mwake.

Tumbo ni mahali ambapo chakula kinameng'enywa ili kuweze kuchukuliwa na mwili ili kuujenga.

Kiroho tumbo ni mchakato ambao unageuza neno tunalolisoma kuwa sehemu ya maisha yetu na huo mchakato ni mchungu.

Kila nabii kabla hajaweza kutabiri kwa mamlaka, nguvu na uvuvio ni muhimu hilo neno la Mungu analotabiri liwe sehemu ya maisha yake yeye katika kuliishi.

Nabii habebi tu ujumbe wa Mungu bali yeye mwenyewe pia ni huo ujumbe.

Ndiyo maana Yesu alisema tutawatambua kwa matunda yao.

Huduma tano teule zinatofautiana tu katika neema ya kuhudumu ila zote zimeitwa kulihudumu neno la Mungu.

Kwa sababu ya zilivyo zitatofautiana neema ya kulihudumu hilo neno kwa sababu ya kusudi na sababu za kuwekwa kwake katika mwili wa Kristo.

Huduma inayodai ni ya kinabii na haihudumu Neno la Mungu bali imejikita kwenye ishara miujiza na maajabu sio huduma halisi ya kinabii ya Agano Jipya.

Ishara miujiza na maajabu ni moja ya vitu ambavyo huduma feki za kinabii zinatumia sana kuwadanganyia watu maana hata huduma halisi ya kinabii inatakiwa kuwa na ishara miujiza na maajabu.

Ila utaigundua huduma feki ya kinabii kwa sababu haipo vizuri kwenye neno maana ni neno tu peke yake ndo linaweza kuwabadilisha watu kitabia na kimwenendo.

Ni neno tu peke yake ndo lina uwezo wa kuleta mabadiliko ya kitabii na kimwenendo kwa watu wa Mungu ila huduma ya kinabii halisi kwa sababu ya unyeti wake na sababu yake ya kuwepo kwenye mwili wa Kristo inahitaji ishara, miujiza na maajabu viambatane nayo kulithibitisha lile neno linalohubiriwa na kufundishwa.

Nabii wa Agano Jipya ni mhubiri na mwalimu mzuri wa neno.

Tofauti yake kubwa ni kwamba analisema hili neno kwa kina cha ufunuo ambao unasababisha mabadiliko ya kitabia na kimwenendo kwa watu wa Mungu.

Huduma ya neno ya nabii wa Agano Jipya inaleta utisho wa Mungu miongoni mwa watu wa Mungu na kukuza utakatifu miongoni mwa watu wa Mungu.

Matunda au matokeo ya huduma halisi ya kinabii miongoni mwa watu wa Mungu ni badiliko la kitabia na kimwenendo ikiwa ni pamoja na kudhihirisha utakatifu kimwenendo na kitabia kwa watu wa Mungu.

Nabii anafanya kazi pamoja na huduma zingine zile nne ili kumfunua Kristo kwa kiwango ambacho anaumbika ndani ya watu na watu wanamfanana Kristo kitabia na kimwenendo.

Kama huduma ya kinabii haifanyi hayo haijalishi kiwango cha nguvu, ishara, miujiza na maajabu hiyo huduma ya kinabii ni feki na sio huduma ambayo ameitoa Yesu kwa Kanisa Lake.

“Tena Yuda na Sila, kwa kuwa wao wenyewe ni manabii, wakawausia ndugu kwa maneno mengi, wakawathibitisha.” (MDO 15:32 SUV).

Manabii wana neema ya kutuusia ili kututhibitisha katika imani.

Kama upo chini ya huduma ambayo unadai ni ya kinabii na hakuna badiliko kwako ya kitabia na kimwenendo, unachapa tu dhambi kama kawaida ujue hujakutana na huduma halisi ya kinabii mpendwa.

Kwa hiyo kigezo kikuu cha kupima huduma ya kinabii halisi ni huduma ya neno.

Ni rahisi sana kuiga na kuzalisha miujiza feki, ishara feki, maajabu feki na nguvu feki ila ni ngumu sana kuzalisha fundisho feki bila kugundulika.

NEEMA NA AMANI ZIZIDISHWE KWENU.

MWALIMU CARLOS RICKY WILSON KIRIMBAI.

WHATSAPP #: +255786312131.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.