SOMO: UNDANI WA MAOMBI (14 & 15) - MCHUNGAJI MADUMLA

Kusoma sehemu iliyopita Bonyeza hapa

06.MAZINGIRA YAFAAYO KATIKA MAOMBI.

Bwana Yesu asifiwe…

Ilikuwa siku moja jioni nilipokuwa nikitoka kazini (maana niliajiriwa kabla ya kuwa mchungaji) nikapata msukumo wa kumuombea mdogo wangu aliyekuwa Afrika ya kusini. Siku hiyo Roho alinisukuma nipambane na kila roho ya uadui iliyomuinukia.

Kumbe siku hiyo hiyo naye alikuwa yupo katika kona mbaya ameachwa na mwenyeji wake,hajui cha kufanya na hana pesa yoyote wala hakuwa na simu, kwa ufupi; alikosa msaada wa kibinadamu.

Nami nikaomba saa ile ile,kisha Bwana alifanya njia kwa ndugu yangu akapata msaada. Nikajifunza kumbe muda wa maombi ni sasa sio kesho,pale unapopata mzigo/msukumo wa maombi ndio hapo hapo pa kuomba.

Hivyo;Ninapozungumzia mazingira yanayofaa kwenye maombi nina maana ya maeneo gani mazuri utakayoyatumia wakati wa maombi yako. Lakini awali ya yote ni lazima tujue kwamba Roho mtakatifu hana mipaka wala hafungwi kwa mazingira yoyote yale. Tukilijua hilo litatusaidia sana haswa tunapoyaangalia mazingira ya maombi.

Eneo zuri lifaalo katika maombi ni mahali popote pale ambapo ndani yako unapata msukumo wa maombi.~ Inawezekana ukawa katika kiwanja cha mpira wa miguu mahali ambapo kuna fujo za kila aina,lakini eneo lilo hilo ndipo gafla unapata msukumo wa maombi,basi ukiona hivyo ujue huo ndio muda muafaka wa kuingia katika maombi pasipo kuangalia mazingira uliyopo.

Mfano mwingine;Unaweza ukawa upo toilet/msalani, lakini gafla ukapokea mzigo wa maombi,basi ujue unatakiwa uingie katika maombi saa hiyo hiyo bila kuchelewa na ikiwa hujui utaomba nini,anza kumuuliza Roho mtakatifu,Naye atakupa cha kuombea,kwa maana Yeye ni mwaminifu Naye husema hata leo.

Wakristo wengi wamekwama katika eneo hili,kwa sababu pale wapatapo mzigo wa maombi wengi hawahushughulikii kikamilifu kwa muda uliotolewa, bali wengi husubiri wafanye kwa muda wao. Ikiwa utapokea ujumbe wa kufanyia kazi leo,nawe ukaupuuzia kisha ukapanga siku nyingine ya kuushughulikia basi ujue itakughalimu sana.

Ni kama vile ukipewa chakula kisha usile leo ukakiacha mpaka siku nyingine labda siku tatu zijazo au wiki moja ijayo ndio ule,basi ujue kitakuwa kipolo kilichoharibika. Viporo vingine utavipasha moto,lakini vingine havipashiki.

Ukiwauliza watu wengi waliopata mzigo wa kuomba kisha wakapuuzia watakuambia madhara waliyoyapata. Ndiposa nikagundua kwamba;hatujui muda muafaka wa kuomba tena wengi hatujui ni mazingira gani yatupasayo kuongea na Mungu. Jifunze kwa Hezekia mtu aliyepewa taharifa ya kutengeneza mambo ya nyumba yake kwa maana atakufa. Biblia inatuambia Hezekia aliomba pale alipopata ujumbe(Isaya 38:1-6).

Hivi,jiulize Hezekia angelifanya kama wengi wafanyavyo leo kupuuzia ujumbe wa Mungu,alafu labda angelisema “Aah,nitamkumbusha Mungu kesho...” Unafikiri angelipona? Au ingelikuwaje? Kumbe yafaa kuomba saa ile ile penye ujumbe wa Mungu,au penye msukumo.

~Hivyo mazingira ya Roho si mazingira ya kwako,ratibz zake si ratiba zako. Lakini ni ukweli kwamba tunazo ratiba zetu tulizojiwekea za kukutana na BWANA MUNGU kwa njia ya maombi.

Ikumbukwe;

kila eneo limebeba hali yake ya kiroho. Mfano;hali ya kiroho iliyopo nyumba za wageni/gesti ni tofauti kabisa na hali ya kiroho ya kanisani. Hivyo ratiba za maombi mazuri zinapaswa kukamilishwa katika mazingira yafuatayo;

(i) Kanisani;

“Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.” Luka 18:10

Kanisani ni eneo la utulivu sana,mahali pa kukutana na Bwana. Eneo hili la hekalu limejaa upako usio wa kawaida,kwa maana ardhi ya kanisa haijabeba laana bali baraka.

(ii)Kambi za maombi.

Ni eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya maombi,siku zote huwa ni eneo la faragha mbali na maeneo ya nyumbani. Yesu nae mara nyingi alitumia muda wake kujitenga na wengine,kisha kupanda mlimani ili kuomba; “ Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.” Mathayo 14:23

(iii) Nyumbani eneo la faragha.

Eneo la nyumbani kwako pia linafaa kwa ajili ya kufanyia maombi. Lakini tafuta sehemu tulivu mahali ambapo hakuna usumbufu wa makelele ya muziki au purukushani zozote. Angalia jinsi ambavyo nyumbani kwa Mariamu palivyotumika kwa ibada za maombi

“Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. ” Matendo 12:12


07.MAZINGIRA YASIYOFAA KATIKA MAOMBI.

Bwana Yesu asifiwe…

Mazingira haya ni mazingira hatarishi hususani kwa jinsia mbili tofauti yaani jinsia ya kike na ya kiume. Mfano si vyema kufanya maombi ndani ya chumba chenye mwanga hafifu,chumba tulivu hivi! hali ninyi si mke na mume.

Au si vyema kwenda kwenye kambi ya maombi ya watu wawili tu mwanamke na mwanaume hali si mke na mume. Ninajua inawezekana wote mkawa rohoni,lakini kumbuka kwamba kwa sehemu bado mnaishi ndani ya mwili,naye shetani yupo akicheza na tamaa za mwili,hivyo ni rahisi kudondoka dhambini. Na hayo ndio mazingira ninayoyazungumzia leo.

Mlokole mmoja alinisimulia kwamba alikuwa akifanyaga maombi na binti mmoja ( Sasa ni mke wake tayari). Walianzia maombi uwani kisha baada ya muda wakasogea sogea sebureni,wakawa wanaomba na kuimba tenzi za rohoni huku wakinena kwa lugha mpya,yani kama vile uonavyo vile tuwapo kanisani.

Unajua tena,maombi yakiwa marefu sana inafika wakati mwili unagomaga,na kama hauko vizuri kiroho basi ni rahisi kutekewa na mazingira ya mwili. Ilikuwa inafika wakati wakichoka kuomba wanapumzika kuvuta pumzi,wakijisomea biblia mara TV kidogo kwa mbaliii. Sasa,kijana akawaka tamaa,lakini alijizuia kwa maana alijiua ni dhambi.

Unajua mazingira waliyokuwepo yalichochea tamaa za mwili ndani yao hata kama wapo rohoni,ilibidi warudi kidogo mwilini. Angalia,binti akiwa amechoka,huenda bafuni kuoga kisha hurudi ndani,akijifuta futa maji,then wanaendelea kuomba.

Pata picha sasa mazingira kama hayo!! Tamaa ikawazidi hatimaye wakaanguka dhambini,wakalala pamoja,lakini si kana kwamba walikuwa wamepanga kulala,ila basi tu mazingira yaliwalazimisha.

Huo ni mfano mdogo tu,ipo mifano mingi inayofanana na hiyo. Wapo watu ambao waliingia dhambini si kwa kupenda bali mazingira waliyokuwa nao yaliwalazimisha,mfano ;wao walikuwa wanaomba lakini mwisho wa maombi mara wakaanguka. Mazingira hayo yote ni mazingira yasiyofaa kwa mwombaji na lazima uyajue hayo.

Haifai kabisa kwa mwombaji kufanya maombi ndani ya geto na binti. Au kuwa na mizaha mizaha na jinsia iliyo tofauti,mizaha ni dhambi (Zab.1:1). Kuna watu wanataniana too much mpaka kero!!!

Tena huyafanya haya yote kabla ya maombi,kisha baadae ndio wanaomba. Haya ni mazingira mabaya kwa maana hakuna maombi ya kweli penye mizaha.

~Epuka mazingira ya mizaha wakati wa maombi.

Utakuta waombaji wakizungumza mambo yasiyowafaa baada au kabla ya maombi. Mazingira haya hukwamisha maombi yako mpendwa. Mfano; waombaji wanaoshindwa kuuzuia ulimi wao,wakitaniana wengine wakisengenya,tena wakimsengenya kiongozi wao mchungaji mkuu. Wakirusha maneno ya kejeri. Au baada ya maombi,utakuta waombaji wakizogoa umbeya N.K. Hayo ni mazingira mabaya.

~Maeneo yoyote yasiyotulivu.

Ukweli ni kwamba mwombaji aweza kuomba eneo lolote,likini hata hivyo bado haupaswi kufanya maombi mahali pa fujo fujo,kwa sababu hakutakuwa na umakini wa kumaanisha kwa kile utakachokuwa ukiomba.

09. SABABU ZA KUTOJIBIWA MAOMBI YAKO.

Zipo sababu nyingi zinazotuzilia majibu ya maombi yetu. Kile ambacho nikijuacho ni kwamba,Mungu anatutaka tumuombe Yeye,ili tupokee. Mungu ametuahidi kutujibu maombi yetu kwa maana Yeye hutusikia tuombapo,( Mathayo 7:7)

Lakini shida iliyopo ni sisi wenyewe tumekamatwa na sababu nyingi mno zinazotufanya hatujibiwi.

Lakini ikumbukwe kwamba njia za Mungu zipo tofauti na za mwanadamu,Yeye hujibu kwa wakati wake

“Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” 1 Petro 5:6

Ingawa ipo hivyo;lakini bado zipo sababu zinazotuzuilia majibu ya maombi yetu,baadhi ya sababu hizo ni kama ifuatavyo;

(i) Upungufu wa imani.

Neno “pungufu “maana yake isiyotimilika,iliyopungua. Hivyo imani pungufu ni imani haba,ni imani yenye mashaka fulani. Upungu wa imani ni mojawapo ya sababu kubwa inayozuia majibu ya maombi yetu. Haimanishi mtu mwenye imani haba hana imani,hapana;

mtu mwenye imani haba ni yule mwenye imani lakini hana uhakika ya mambo anayoyatarajia. Tujikumbushe habari ya wanafunzi wa Yesu waliposhindwa kupata majibu yao kwa sababu ya ungufu wa imani.

“ Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya.Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu…“Mathayo 17:16 & 20a

Wanafunzi wa Bwana,walikuwa na imani lakini imani yao haikuwa na uhakika wa uponyaji;hawakuweza kumponya kwa sababu hiyo. Waombaji wengi wamekwama eneo hili,kuomba wanaomba lakini hawaamini sana kile walichoomba.

Utakuta mwombaji anaombea kuhusu ndoa yake,lakini alafu anajiuliza “ hivi kweli mume wangu atabadilika? Mmhh yaani naona haitawezekana,maana kila kukicha ni ugomvi...”

Kwa mfano huo,inaonesha kwamba muombaji ana mashaka na uponyaji wa ndoa yake. Sasa angalia kile kinachotokea,majibu hayaji kwa maana mwombaji amejawa na mashaka. Hakikisha una imani timilifu pale uombapo,amini kwamba kile ukiombacho umepokea tayari…

Kwa huduma ya maombezi piga sasa; 255 655 111 149,+255 684 033 334 au +255 762 414 446. 
ITAENDELEA…
Mchungaji Gasper Madumla,
Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ),
UBARIKIWE.


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.