FALSAFA YA IMANI KWA MUJIBU WA AGANO JIPYA


Askofu Sylvester Gamanywa.

“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” (Rum.10:17)

Mpendwa msomaji wangu! Je unaona ujumbe uliomo katika maandiko niliyonakili hapa juu? Ujumbe unasema kwamba, chanzo cha imani itendayo kazi ni kutokana na “Neno la Kristo”! Sio “Neno la Musa” wala sio “Neno la Eliya” Ukomo wa mafunuo ya Musa na Eliya ulikuwa ni ujio wa Yesu Kristo duniani ambapo alitambulishwa na Baba yake akisema: “huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.” (MT.17:5)

Imani ya kutuokoa, kutuponya na kubariki kiroho, kijamii, na kiuchumi inazaliwa na kujengwa kwenye maneno yaliyotoka kinywani mwa Yesu anaagiza tuyashike hayo. Kabla sijaenda kwenye kina cha ujumbe wangu nataka mimi na wewe tujiulize bila unafiki. Hivi kama kweli Yesu tunayemwamini hivi leo ni “yeye yule jana na leo na hata milele” ni kwanini kazi zake alizoahidi kwamba zitaendelea kufanyika mpaka atakaporudi hazifanyiki kwa viwango vile vile vya mitume na wakristo wa karne ya kwanza?

Na kama kweli Roho Mtakatifu ambaye tunampokea na kujazwa naye enzi hizi ndiye yule yule aliyetumwa na Yesu na kujidhirisha waziwazi kupitia wakristo wa karne ya kwanza; ni kwanini enzi zetu bado hajidhihirishi kwa viwango vile vile vya karne ya kwanza?

TUNAISHI KWENYE KIZAZI KILICHOKENGEUKA KIIMANI

Sitaki kumung’unya maneno katika kujibu maswali haya. Majibu yake ni kwamba, sisi tunaishi katika enzi za ukengeufu wa imani kama ule wa kizazi cha Wagalatia ambao “walianza katika Roho kisha wakakengeuka na kutafuta kukamilishwa katika mwili.” (Gal.3:3)

Ukifuatilia msisitizo na uzito wa mafundisho na mafunuo ya leo utagundua vimejikita kwenye manabii wa Agano la Kale, akina Musa na Eliya, ambao Mungu alikwisha kusema tumsikilize Yesu badala hao. Sehemu kubwa ya mahubiri, mafundisho, hata mtazamo wa baraka za kiuchumi tumeelemea kanuni na sheria za Agano la Kale. Hata kizazi cha manabii wa leo kinatabiri na kufuata mtindo wa manabii wa Agano la Kale.

Sisemi kwamba maandiko ya Agano la Kale sio neno la Mungu. Hoja yangu ni kuweka bayana kwamba Agano la Kale limebaki kwetu kuwa ni historia; lakini halina maneno ya imani iliyoanzishwa na Yesu Kristo na kuhubiriwa na mitume wa karne ya kwanza. Kwa mantiki hii tunaendeleza kizazi kilichokengeuka kiimani kutoka kwenye msingi wa Agano Jipya na kurejea katika Agano la Kale.

Wakati maneno ya imani yenye kuokoa roho zetu hayamo katika Agano la Kale bali yamo kwenye Agano Jipya. Ndiyo maana hatuzioni nguvu za Roho Mtakatifu kama zilivyokuwa nyakati za Mitume wa kwanza. Tunatafuta na kuamini maandiko ambayo si ufunuo wa waliofanyia kazi mitume wa kwanza. Ndiyo maana tuko nyuma ya viwango vya imani ya wakristo wa karne ya kwanza.


USHAHIDI WA KIMAANDIKO KUHUSU IMANI YA AGANO JIPYA

Ngoja nikupe ushahidi wa kimaandiko. Nikupe tu mfano mdogo wa msamiati wa maneno “imani” na “kuamini” katika Biblia. Katika Agano la kale utakuta maandiko yanayotaja “Imani na kuamini” mara 19 tu; ambayo ni 4.% ya maneno yote kuhusu imani na kuamini katika Biblia nzima. Ukija kwenye Agano jipya utalikuta limetaja manenoya “imani na kuamini” mara 425 ambayo ni sawa na 96% ya Biblia nzima.

Kana kwamba hii haitoshi, hebu nikuingize kwa kina katika kuyachunguza chimbuko la maneno ya “imani na kuamini” humu humu kwenye Agano Jipya. Yesu Kristo ndiye aliyetangulia kusema kwa habari za “imani” na “kuamini” katika Agano Jipya.

Nikufahamishe kwamba, katika Agano Jipya, kuna mistari ya maandiko matakatifu ipatayo 7,959. Kati ya mistari hiyo kuna mistari 1,599 ambayo ni maneno ya Yesu mwenyewe ambayo ni sawa na 20% ya maandiko yote katika Agano Jipya. Haya tukija kwenye misamiati ya maneno ya “imani na kuamini” utamkuta Yesu alisema mara 141 ambayo ni sawa na 31.75% ya maandiko yote katika Agano Jipya.

Ushahidi mwingine wa tafiti za kimaandiko unatufundisha kwamba, Paulo aliteuliwa kuwa mtume wa mataifa, yaani jamii ya watu ambao si wayahudi na ambao kwa asili hawakuwa na shehemu yoyote katika Agano la Kale. Huyu mtume Paulo namwita “Mtume wa Imani”! Yeye ndiye aliyemwamini Yesu kama vile Yesu alivyoahidi kwamba amwaminiye yeye hata kazi za Yesu atazifanya na kubwa kuliko hizo atazifanya.

Ngoja nikupe ushahidi wa kimaandiko kuhusu Paulo. Katika Agano Jipya mtume Paulo amefundisha kwa maandiko matakatifu kuhusu misamiati ya maneno “imani na kuamini” kwa kuyataja mara 215 ambayo ni sawa na 48.42% ya maandiko yote ya imani katika Agano Jipya. Yaani karibu nusu ya maandiko ya Agano Jipya kuhusu imani imeandikwa na Paulo.

Ndiyo maana tunasoma kwamba “Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida" (Mdo.19:11). Maana yake Paulo alikuwa ameshika imani kubwa kupita kawaida, na ndiyo maana akaandika habari za imani kwa wingi kupita kawaida ya wengine wote waliomtangulia.

Huu ni ushahidi mwingine ulio dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya fundisho la imani kwa Mungu katika Biblia nzima limejengwa kwenye Agano Jipya na sio Agano la Kale.

Nitaendelea na makala haya sehemu ya pili inayokuja. Leo nataka tuyatafakari haya kwanza. Tafadhali kama umebarikiwa na ujumbe huu warushie na marafiki zako wote na kuwaalika tukutane kwenye sehemu ya pili ya ujumbe huu.

Humo nitafafanua ni jinsi gani sisi tanatakiwa kuondoka kwenye ukengeufu na kurejea kwenye Agano lililo bora lenye ahadi zilizo bora ili tuyaishi maisha yaliyo bora kiimani kama wakristo wa karne ya kwanza. Ubarikiwe sana!

Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.