MAKALA: FALSAFA YA IMANI KWA MUJIBU WA AGANO JIPYA (2)

Askofu Sylvester Gamanywa
Naomba kuchukua fursa hii kuwasilisha sehemu ya pili ya makala ya FALSAFA YA IMANI KWA MUJIBU WA AGANO JIPYA. Najua kwa wengine itakuwa imechelewa lakini nilitaka ya kwanza iwafikie angalau wengi zaidi kabla sijarusha sehemu ya pili.

Kwa wasomaji wapya nianze kwa kurejea kwa kifupi makala sehemu ya kwanza (soma hapa) ilikuwa na maswali magumu yenye kuhoji ya kwamba “kama Yesu tunayemwamini sisi hivi leo ni yule yule wa Wakristo wa Karne ya kwanza; ni kwanini kazi zake hazifanyi kwa viwango vile vile vya wakristo waliotutangulia katika imani? Na Roho Mtakatifu tuliye naye hivi leo ndiye yule yule wa karne ya kwanza ni kwanini hajidhihirishi kama alivyofanya kwenye matendo ya mitume?"

Katika kujibu maswali hayo, nilidokeza kwa kifupi ya kwamba sisi “tunaishi kwenye kizazi kilichokengeuka kiimani” kwa sababu tumeliacha Agano Jipya na tumerejea kwenye Agano la Kale. Tumeacha kumsikiliza Yesu ambaye Baba alituagiza tumsikilize yeye tumewageukia akina Musa na Eliya ambao huduma zao zilikwisha kuchukuliwa na huduma ya Yesu Kristo.

Mstari wa Warumi 10:17 ambao ulikuwa ndio ufunguo wa makala iliyopita ulilenga kutukumbusha kwamba, siri ya imani itendayo kazi kama ile ya mitume lazima chimbuko lake liwe ni “Neno la Kristo” na si “Neno la Musa” na wala si “Neno la Eliya.”

Katika sehemu hii ya pili, napenda kujenga misingi ya kutuongoza kuirejea imani ya Agano Jipya kwa kubainisha tofauti zilizopo katika Agano la Kale na Agano Jipya. Nataka tujifunze kwa mujibu wa tafsiri za kimaandiko ni kwanini tunatakiwa kujijenga kiimani kwenye maneno yaliyomo katika Agano Jipya kama kweli tunataka kuzishuhudia nguvu za Roho Mtakatifu wa karne ya kwanza.

TOFAUTI KATI YA AGANO LA KALE NA AGANO JIPYA

Madhumuni ya uchambuzi huu sio kubagua kati ya agano lipi ni bora zaidi ya jingine! Madhumuni ni kuweka bayana nafasi na kazi ya kila agano ili sisi tupate kujua tunahusika vipi na kila agano! Ni kweli kabisa kuamini kwamba maandiko matakatifu yaliyomo katika maagano yote mawili ni maandiko yaliyo vuviwa na Roho Mtakatifu na kwa hiyo yote ni neno la Mungu! Yote yanafaa kwa fundisho na maonyo na mwongozo wa kiroho kwa mchaji Mungu

Jambo muhimu la kuwa makini ni kufahamu ya kwamba si kila andiko katika kila agano linahusuka kwa watu wote, mahali pote na wakati wote! Yako baadhi ya maandiko matakatifu ambayo yana walengwa maalum wa mahali tofauti na nyakati tofauti! Kwa mantiki hii kila Agano katika Biblia katika maana yake sahihi lina ujumbe maalum kwa walengwa maalum, na kwa nyakati tofauti!

VIGEZO VYA TATHMINI

Kabla sijaingia kwa kina kwenye makala hii, naona ni muhimu nitoe utetezi ni kwanini ninasisitiza ya kwamba, tunatakiwa "kurejea kwenye msingi ya agano jipya" ambalo ndilo mafunuo yake yana tija kwa imani yetu; badala ya kutafuta mafunuo kwenye historia ya mafunuo ya kale. Maandiko yenyewe yatatuthibitishia uzito uliopo kati ya Agano Jipya na Agano lake. Nimechagua vigezo 6 tu vya kutusaidia kufanya uchambuzi ambavo ni kama ifuatavyo:

1. Kigezo cha Walengwa

KIgezo hiki kinatufunulia ni akina nani ni walengwa wakuu wa kila agano. Agano la Kale walengwa wake ni Taifa la Israeli ambalo ni makabila 12 ya uzao wa Yakobo. Ahadi, baraka na masharti yaliyomo katika Agano la kale yalikuwa ni kwa ajili ya wana wa Israel. Mataifa mengine ambayo si wayahudi hayakuwa na sehemu katika Agano hilo, na ndiyo hata kutajwa kwao kuna kiwango cha 2.8 peke yake, wakati Israeli imetajwa kwa 97.1%

Walengwa wakuu wa Agano Jipya ni Kanisa. Hii ni taasisi mpya ya kiroho iliyoanzishwa na Yesu Kristo na ambayo ni mjumuiko wa Israeli pamoja na mataifa yote waliomwamini Yesu. Kimsingi ni kwamba, Yesu Kristo alifanya agano jipya kwa ajili ya ulimwengu mzima!

Agano la kale kazi yake ilikuwa ni Kuwakomboa wana wa Israeli toka Misri wapate kurithi nchi ya ahadi ya Kanaani! Agano jipya ni kuwakomboa mataifa yote kutoka utumwa wa dhambi na kuwafanya wanafunzi kwa kuwabatiza na kuwafundisha kuyashika yote aliyoamuru Yesu Kristo.(Mt.28:19-29) Ndiyo hata neno wanafunzi linapatikana katika Agano Jipya kwa 99% na katika Agano la Kale 1% tu!

Neno kanisa halikutajwa kabisa katika Agano la Kale, na badala yake limejaa kwenye Agano jipya kwa 100%. Hata neno “mataifa” limetajwa katika Agano la Kale kwa kiwango cha 23.2% wakati kwenye Agano jipya limetajwa kwa kiwango cha 76.7%.

Huu wote ni ushahidi kamili kwamba Agano la Kale walengwa wake ni Israeli na Agano Jipya walengwa wake ni Kanisa ambalo ni mjumuiko wa Israeli na mataifa yote ulimwenguni waliomua kumwamini Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wao

2. Kigezo cha dhabihu

Agano la Kale limejengwa kwenye dhabihu za damu ya wanyama kwa ajili ya kufunika dhambi za wana wa Israeli. Neno “dhabihu” limetajwa mara 217 katika Biblia. Aidha, neno dhabihu limetajwa kwenye Agano la Kale mara 185 ambayo ni sawa na 85.2% ya maneno yote ya Biblia. Wakati kwenye Agano Jipya neno dhabihu limetajwa mara 32 ambao ni sawa na 14.7% ya maneno yote ya Biblia.

Huu ni ushahidi usiopingika kuonyesha kwamba kazi ya Agano la Kale ilikuwa ni kutoa dhabihu mara kwa mara, kila mwaka; wakati kwenye Agano Jipya "dhabihu iliyo kamili imetolewa mara moja tu ambayo ni damu ya Yesu Kristo". Dhabihu nyingine katika agano jipya ni dhabihu za kiroho tu.

3. Kigezo cha utii na uasi

Agano la Kale lilijengwa kwenye sheria ya utii na uasi! Maana yake kutii sheria ndiyo kigezo cha kukubalika na kubarikiwa wakati kuasi sheria matokeo yake ni hukumu ya adhabu kulingana na sheria iliyovunjwa!

Nabii Isaya anathibitisha haya alipoandika akisema: "mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; lakini mkikataa na kuasi mtaangamia kwa upanga, maana kinywa cha BWANA kimenena haya" (Isa. 1:19-20) Ndiyo maana neno "uasi" kwenye Agano la Kale limechukua sehemu kubwa kiwango cha 89.2% tofauti na Agano Jipya ambamo "uasi" limetajwa kwa 10.7% tu

4. Sheria ya torati na injili ya neema

Agano la Kale ni Agano la Sheria. Katika Biblia neno sheria au torati limeandikwa mara 523. Kwa kiasi hiki Agano la Kale limechukua maneno 300 sawa na 57.3% ya maandiko yote ndani ya Biblia. Katika Agano Jipya neno sheria limetajwa mara 223 ikiwa ni sawa na 42.6% ya idadi ya maneno yote katika Biblia. Kwa mantiki hii, ndiyo maana Agano la Kale latafsiriwa kuwa ni la sheria zaidi kuliko Agano Jipya.

Neno “neema” limeandikwa katika Biblia mara 170. Katika Agano la Kale neema imetajwa mara 60 tu sawa na 35.2%, wakati kwenye Agano Jipya neema imetajwa mara 110 ambayo ni sawa na 64.7% ya maneno yote ya Biblia.

Neno “Injili” limeandikwa mara 101 katika Biblia. Katika Agano la Kale hamna neno Injili hata mara moja. Agano Jipya ndilo peke yake linalotupa neno “Injili”. Kwa hiyo, Agano Jipya ni agano la Neema ambayo ujumbe wake ni Injili ya Neemaambayo asili yake ni Yesu Kristo mwenyewe.

5. Kigezo cha kuamini na kutokuamini

Kauli mbiu ya Agano Jipya ni tofauti na Isaya! Yesu anaagiza kwamba "aaminiye na kubatizwa ataokoka asiyeamini atahukumiwa" (Mk.16:16) kwa hiyo kuamini au kutokuamini ndiyo mfumo wa Agano Jipya!

Ndiyo maana neno "imani" pamoja na "kuamini" yamejaa kwa 95.1% wakati kwenye Agano la Kale ni 4.8% tu! Neno "kutokuamini" halikutajwa kabisa katika Agano la Kale kwa sababu halikuwa agano la imani bali la torati!

6. Kigezo cha baraka na laana

Neno “baraka” limechukua nafasi kubwa katika Agano la Kale kwa kiasi cha 89.3% wakati kwenye agano jipya baraka limetajwa kwa kiwango cha 10.7%. Ukifanya majumuisho ya baraka na laana utapata kiwango cha 89.5% na kwenye Agano Jipya ni 10.5% tu

Ni nini tunajifunza katika eneo hili? Agano la kale baraka na laana zake zilikuwa ni za kimwili 100%; wakati baraka la laana za Agano Jipya ni za kiroho. Ndiyo maana inakuwa rahisi kushawishika kurejea kwenye Agano la Kale kwa ajili ya kutafuta baraka za kimwili na kupuuza baraka za kiroho ambazo zimejengwa kwenye misingi ya kiroho.

Kwa kukwepa kuamini na kutendea kazi baraka za rohoni ambazo zimo ndani ya agano jipya; wengi hukimbilia kwenye agano la kale kwa ajili ya kutafuta baraka za kimwili. Matokeo yake wanakosa vyote. Hizo baraka zenyewe za kimwili hawazipati na wakati huo huo hata baraka za rohoni hawazipati kwa sababu wanatafuta baraka za kimwili tu.

Makala hii itaendelea sehemu ya tatu ambapo nitarejea kuweka waziwazi baraka za kiroho za agano jipya ni zipi? Je hazihusiki na baraka za kimwili kama agano la Kale? Tafadhali nisaidie kuwarushia marafiki zako ujumbe huu ili waweze kujumuika nasi katika sehemu ya tatu ambayo humo ndimo kiini cha ujumbe huu kitawekwa bayana. Ubarikiwe sana.

Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.