MTOTO WA MIAKA 12 AOKOLEWA NA SIMBA MIKONONI MWA WATEKAJI

Picha ya Mtandao

Kwa kawaida ukiwa mwituni na ukamuona simba, utafurahi kama uko kwenye utalii. Lakini iwapo simba huyo anajongea kwako ama mazingira ya nyumbani kwako, basi hapo utatambua ya kwamba uko kwenye matatizo makubwa sana. Kwa maana ni ama simba ananyemelea mifugo aichukue, ama mwisho wa siku atadhuru mtu. Muungurumo wake tu unaweza kuhisi kuchafukwa na tumbotayari.

Lakini kwa wasomaji wa Biblia, kuna ile habari ya Daniel kutupwa katika tundu la simba, hakika utatambua kwamba ni Mungu pekee anayeweza kunusuru kwa namna ile, kama ambavyo mfalme Dario alivyosadiki ya kwamba Mungu wa Danieli ni wa kweli hakuna mwingine. (Danieli 6:1-28)

Nchini Ethiopia imerioptiwa tukio la ajabu na la kipekee, na hili ni tukio la binti wa miaka 12 kulindwa na simba dhidi ya watesi wake. Na si kwamba simba hao amewafuga yeye ama ni wa nyumbani kwao, La Hasha! Hakukuwa na undugu wala urafiki baina yao. Tukio hili limeripotiwa mwaka 2005, lakini limekuwa likizunguka mitandaoni mara kwa mara. Tunakufahamisha.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press (AP), mtoto huyo (jina lake limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 12 alitekwa nyara na kupigwa na wanaume saba, ambao walikuwa wakimlazimisha aolewe, katika tukio ambalo limetokea mapema mwezi Juni mwaka 2005.

"Mtoto huyo aliyetoweka kwa takribani wiki moja, alitekwa na kulazimishwa akubali kuolewa na mwanaume mmoja miongoni wa watekaji wake." Sajenti Wondimu Wedajo anaeleza kwa njia ya simu kutoka Bita Genet, takriban kilomita 560 Kusini Magharibi kutoka Mji Mkuu wa Addis Ababa.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba binti huyo alipatikana Juni 9 mwenye majeraha ya vipigo vya watekaji wake, ambapo simba watatu walikuwa wakimlinda kwa masaa zaidi ya nane baada ya kuwafukuza watesi wake, hadi msaada ulipopatikana.

Kwa mujibu wa Tilahun Kassa, mmoja wa viongozi wa serikali za mitaa, anaeleza kwamba matukio mengi hutokea ya watoto wa kike kutekwa, kuteswa, kubakwa na kisha kulazimishwa kuolewa, lakini kwa kilichojiri ni muujiza.

"Kila mmoja anadhani kilichotokea ni muujiza, kwa maana kikawaida simba hawa wangeshamshambulia binti huyu" Anaeleza Kassa.

Simba hao walikaa pamoja na mtoto huyo hadi polisi na ndugu walipofika eneo la tukio, ndipo simba hao watatu wakaanza kuondoka polepole kama vile walijua nini kinaendelea. Hakuna madhara yaliyoripotiwa kutokana na simba hao. Sajenti Wedajo alimaliza kusimulia.

Aidha akieleza jambo hilo kitaalamu, mtaalamu wa wanyamapori kutoka wizara ya maendeleo ya vijiji (rural development minsitry), Stuart Williams, anasema kwamba huenda mtoto huyo amepsalimika kutokana na kilio chake, na hivyo simba wakamuacha kwa kufananisha kilio chake na sauti ya simba watoto.

Hata hivyo watumiaji wa mitandao ya kijamii wameonekana kuchefukwa na kukashifu wazo la mtaalamu Williams, wakisema kwamba kama ni hivyo basi huenda hata simba hao pia waliifananisha sura ya binti huyo na sura ya simba watoto vinginevyo wangeshamtafuna na si kukaa naye kwa amani.

Watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii waliamua kukiri moja kwa moja ya kwamba ni Mungu pekee ndiye aliyemuokoa mtoto huyo kupitia hao simba, vinginevyo ingebaki kuwa historia tu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, utekaji wa namna hiyo umekuwa wa kawaida nchini Ethipia, ambapo takriban asilimia 67 ya ndoa zote nchini humo zinatokana na utekaji.

Chanzo: BBC News  |  NBC News  |  Guardian  |  Associated Press


Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.