FALSAFA YA IMANI KWA MUJIBU WA AGANO JIPYA (3)

Askofu Sylvester Gamanywa.
Kwenye makala ya sehemu ya pili (soma hapa) nilichambua tofauti kati ya Agano la Kale na Agano Jipya kwa kutumia vigezo 6 vya tathimini ambavyo vilikuwa ni pamoja na: Kigezo cha Walengwa; Kigezo cha dhabihu; Kigezo cha utii na uasi; Sheria ya torati na injili ya neema; Kigezo cha kuamini na kutokuamini na mwisho ilikuwa ni “Kigezo cha baraka na laana”

Sehemu ya tatu ya makala hii kwa kujibu maswali ya uelewa kwenye kujua baraka za kiroho za agano jipya ni zipi na kama zina uhusiano na baraka za kimwili za agano la kale.

UBORA WA AGANO JIPYA

Naomba kwanza kutoa utetezi kuhusu matumizi ya lugha ya “ubora wa agano jipya” kwamba sio mawazo yangu binafsi, bali ndivyo maandiko yasemavyo. Natambua uwepo wa watetezi wa “nafasi ya agano la kale” wenye kusisitiza ya kwamba “ujumbe wa agano la kale” una hadhi na uzito sawasawa na “ujumbe wa agano jipya” kwa kuwa yote ni maandiko matakatifu kwa wote. Napenda kuwajulisha kwamba maandiko yanajitetea na kujithibitisha yenyewe kwa yenyewe yakisema “ubora wa agano la kale” umepitwa na “ubora wa agano jipya.”

Katika Agano Jipya, kazi ya ukombozi wa Yesu Kristo imekubalika mbele za Mungu kuwa “huduma iliyo bora (Ebr.8:6 ); na hivyo kumfanya Yesu kuwa “mdhamini wa agano lililo bora”, tena lenye “ahadi zilizo bora” (Ebr.7:22); Kana kwamba hii haitoshi, maandiko yameweka bayana kwamba kwa ubora wa agano jipya; kudhihirisha upungufu wa agano la kale: “Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili….” (Ebr.8:7)

Na mwisho kabisa maandiko yameweka bayana kuwepo kwa agano jipya kumelifanya agano la kale kuwa chakavu: “Kwa kule kusema agano Jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kiaanzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.” (Ebr.8:13)

UBORA WA AGANO JIPYA UPO KATIKA MISINGI YA KIROHO

Misingi ya kiroho ya agano jipya ni ya kushughulikia shina sugu la tatizo la dhambi ambalo lilimfanya binadamu kuwa mtumwa wa Ibilisi. Kazi ya ukombozi wa Kristo ilifanyika katika ulimwengu wa roho. Na ndiyo maana matunda ya kwanza ya kiroho yanaanza na ngazi ya mtu “kuzaliwa mara ya pili katika roho” (Yoh.3:1-6) Ngazi ya kuzaliwa mara ya pili katika roho humfanya muhusika “kuketishwa pamoja na Kristo katika ulimwengu wa roho;” ( Efe.2:4-6 ) na “kufanyika raia wa mbinguni katika roho.”( Flp.3:20 )

Baada ya Hatua za uzawa na uraia wa mbinguni; kinachofuata ni muhusika ni kupokea “baraka zote za rohoni”(Efe.1:3). Baada ya hayo, huku tukingali bado tuko duniani tunaendelea na zoezi la kiroho ambalo ni “kumwabudu Mungu ambaye ni Roho” (YH 4:23 ) na tulifanya kwa viwango vya “kumwabudu katika roho na kweli”(YH.4:24).Na mwenye kutusaidia zoezi hili kubwa la kiroho la kuabudu katika roho na kweli ni Roho Mtakatifu ambaye hutusaidia udhaifu wetu kwa kuwa hatujuiitupasavyo katika kuabudu, bali yeye hutuongoza kwa kuabudu katika roho ipasavyo (Rum.8:26)

Katika mfumo huu wa maisha ya imani katika agano jipya umejengwa kwenye matokeo ya kazi iliyokwisha kufanyika kwa ajili yetu; na sio kwa matendo yetu wenyewe kama ilivyokuwa kwenye mfumo wa agano la kale. Yafuatayo ni mambo kadhaa ambayo tunayapokea kwa imani katika agano jipya:

1. Kwa imani tunapokea baraka za kiroho kupitia kazi ya ukombozi iliyokamilika kwa kifo na kufufuka kwa Yesu Kristo. Msingi wa baraka za kimwili katika agano jipya ni matunda au matokeo ya baraka za kiroho katika Kristo Yesu. Katika Agano Jipya hatufanyi mambo ya kutufanya tukubalike kwa Mungu kwa kuwa Yesu alifanya yote kwa ajili yetu na kwa njia hiyo akatufanya tukubalike bure mbele za Mungu

2. Kwa imani tunatoa vyote tulivyo navyo kwa ajili ya Yesu Kristo; sio ili turudishiwe vingi kwa maslahi yetu binafsi; bali tufanyike baraka kwa mwili wa Kristo na jamii kwa jumla. Kwa imani tunapokea wajibu wa kuwa mawakili wa mali za Kristo kwa ajili ya injili na huduma za kikanisa; maana yake kipaumbe cha matumizi na kiwango kikubwa cha matumi ya mali na mapato yetu vinahitajika kwenye injili ya Kristo na huduma za kikanisa. (Katika sehemu ya 4 na ya mwisho nichambua utoaji wa agano jipya tofauti na utoaji wa agano la kale.)

UBORA WA AGANO JIPYA UPO KWENYE MISINGI YA UMILELE

Ubora wa aagano jipya unapata uzito zaidi pale ambapo mambo yake na baraka zake ni za milele. Ahadi ya kwanza iliyo kuu ni uzima wa milele kwa kila mwenye kushiriki agano hilo. “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia” (YH.3:36).

Makao ya milele “Nyumbani mwa Baba mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakribishe kwangu; ili nilipo mimi nanyi mwepo.” (YH.14:2-3)

MCHAKATO WA KUPATA MAMBO YA KIROHO

Kupata mambo ya kiroho katika agano jipya kuna mchakato wake kwa kila mwenye kuhitaji. Mchakato wenyewe unazingatia hatua muhimu tatu. Hatua ya kwanza ni “kuamini”. Kwanini kuamini ni lazima? Kwa sababu mambo ya kiroho yanapatika kutoka kwenye ulimwengu wa roho. Na hatuwezi kuingia huko kwa njia ya za kimwili. Njia pekee ya kuingia katika ulimwengu wa ni imani.

Hatua ya pili, baada ya kuamini katika ahadi za Kristo kupitia Neno lake kwenye Agano Jipya, ni “kupokea” kwa imani. Hapa “kupokea” ni hatua ya pili ya matumizi ya imani. Kwanza unapata hakika moyoni kwa ahadi za Kristo ni kweli na kwa ajili yako. Pili, kwa hakika hiyo hiyo unajenga hali ya kupokea kwa wakati huo huo unapopata hakika moyoni.

Kwa hiyo, kuamini (kuwa na hakika moyoni) kunafuatiwa na kupokea kwa wakati huo huo kile ulichoamini. Ndiyo maana watu wote waliomwendea Yesu akasema wamepokea uponyaji na miujiza kwa imani zao; ni kwa sababu walikwisha “kuwa na hakika mioyoni mwao kwamba Yesu Kristo ni mponyaji na mtenda miujiza; na kwa imani hiyo hiyo wakapokea uponyaji na miujiza yao wakati huo huo walipokuwa mbele za Yesu Kristo.

MAJIBU KWA MASWALI YA CHRISTIAN NTEZI

Swali la kwanza ulitaka kujua kama neno KUTOKUAMINI halimo kwenye Agano la Kale. Jibu ni ndiyo, katika Biblia ya Kingereza haijataja neno “unbelief”. Kwenye mistari ambayo inatafsiria kutokuamini kwa Kiswahili kwa kingereza limetumika neno “they did not believe” badala ya neno “unbelief”!

Hata hivyo hoja yangu ya msingi katika eneo hilo nilikuwa nasisitiza kwamba “kutokuamini kwa agano la kale” kulijengwa katika “kutokutii sheria”! Katika Agano Jipya tunahukumiwa kwa “kutokuamini” kwa sababu ahadi na baraka zetu ni za rohoni na zinapatikana katika ulimwengu wa roho.

Kuhusu swali la zaka hilo nitalichambua vizuri zaidi kwenye sehemu ya nne ya makala hii ambayo itakuwa ndiyo hitimisho la mwisho.

PONGEZI KWA WASOMAJI WANGU

Napenda kuchukua fursa kuwashukuru marafiki wasomaji wa page yangu. Nishukuru kwa wengi kufuatilia makala hii ambayo ni ndefu kwa maelezo. Nawashukuru waliowashirikisha marafiki zao wengi ujumbe wa makala hii. Nitashukuru kama nyote mnaosoma mtaweza kuwashirikisha marafiki zenu wengine ujumbe huu. Ni kwa njia hii tunajengana kiimani na kupona na changamoto za kiimani katika ulimwengu huu ulioharibika kimaadili. Mbarikiwe sana
Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.