FALSAFA YA IMANI KWA MUJIBU WA AGANO JIPYA (4)


Askofu Sylvester Gamanywa

MISAMIATI

Kwanza kabisa napenda kutambua na kuheshimu michango mingi ya walimu na watumishi mbali mbali wenye kufundishia na kuhamasisha utoaji kwa ajili ya huduma za Injili katika mwili wa Kristo. Madhumuni ya makala ya leo ni kuchangia (complement) kile ambacho nimejaliwa kuona kwamba kimepungua ili kusaida waamini katika KUIJUA KWELI YOTE.(soma sehemu iliyopita hapa)

Na kabla sijachambua kwa kina kuhusu utoaji katika Agano Jipya, nianze kwanza na tafsiri ya misamiati ya maneno maarufu ambayo hutumika zaidi kuhusu utoaji katika Biblia. Misamiati hiyo ni maneno "Dhabihu” (sacrifices), “Sadaka” (Offerings), “Zaka” (Tithe), “Kutoa” (Give), na “Utoaji” (Giving).

Tuanze na msamiati wa neno "dhabihu” ambalo katika Biblia ya Kingereza (KJV) limetajwa mara 297. Kwenye Agano la Kale limejatwa mara 270 sawa na 90.9%! Na kwenye Agano Jipya limetajwa mara 27 tu sawa na 9.1%. Kwa matokeo haya ni dhahiri neno "dhabihu" limetumika katika Agano la Kale zaidi kuliko katika Agano jipya.

Neno la pili ni “sadaka”! Hili limetajwa mara 989 katika Biblia. Kwenye Agano la Kale limetajwa mara 974 sawa na 98.4% na kwenye Agano jipya limetajwa mara 15 tu sawa na 1.6%. Huu pia ni ushahidi kwamba matumizi makubwa yanaangukia kwenye Agano la Kale kuliko Agano Jipya. Neno la tatu ni “Zaka” (maarufu kwa jina la sehemu ya kumi au fungu la kumi) na limetajwa mara 38 katika Biblia. Kwenye Agano la Kale limetajwa mara 31 sawa na 81.5% na katika Agano Jipya limetajwa mara 7 tu sawa na 18.5%. hili nalo sawa na “dhabihu” na “sadaka” limetumika kwa wingi katika Agano la kale kuliko Agano Jipya.

Neno la nne ambalo ni “kutoa” (Give) na limetajwa mara 880 katika Biblia. Kwenye Agano la kale limetajwa mara 693 sawa na 78.7% wakati kwenye Agano Jipya limetajwa mara 187 sawa na 21.3%. Hapa tumeanza kuona kiwango cha matumizi ya neno “kutoa” kimepanda katika agano jipya kuliko maneno matatu yaliyotangulia ambayo ni dhabihu, sadaka na zaka! Neno la tano na la mwisho ambalo limeongoza katika matumizi kwenye agano jipya kuliko agano la kale ni “utoaji”(giving) ambalo limeandikwa mara 29 katika Biblia. Kwenye agano la kale “utoaji” limetajwa mara 8 tu sawa na 27.5% wakati ambapo kwenye agano jipya limetajwa mara 21 sawa na 72.5%.

Kwa tathmini hii, tumeshuhudia maneno mawili ambayo tinaweza kuyafuatilia kuhusu utoaji wa agano jipya ni "kutoa" na "utoaji"! Haya maneno mengine ya dhabihu, sadaka na zaka yanabaki kuwa ni misamiati ya agano la Kale zaidi kuliko Agano Jipya. Sio makosa wala dhambi kuyatumia kwa kujifunza kihistoria. Lakini tuukubali ukweli ya kwamba katika agano jipya hayakutimika kama fundisho la imani kwa utoaji kwa mkazo wa misingi ya agano la kale.

KIWANGO CHA UTOAJI KATIKA AGANO JIPYA

Katika agano la kale kiwango cha utoaji wa sadaka na zaka kilikuwa ni sehemu ya kumi (10%). Lakini kwenye agano jipya, kiwango cha utoaji kilipanda mpaka 100%! Huu ndio ulikuwa msimamo na fundisho la imani la Yesu Kristo kwa wanafunzi wake. Utoaji wa 100% Misamiati ya maneno ya Yesu kuhusu "kutoa 100%" yalikuwa ni "kuacha vyote" au "kutoa vyote" au "kuuza vyote"!

Isitoshe, kutoa 100% ilikuwa ni sharti maalum la kuwa mwanafunzi wa Yesu, na aliyeshindwa sharti hili "hakustahili kuwa mwanafunzi wa Yesu: “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” ( Luk.14:33) Maneno ya “asiyeacha vyote alivyo navyo” yanatafsiri ya kuacha/kutoa kwa 100%! Unaweza kupata shida katika kuukubali ukweli huu. Lakini ndio ukweli wenyewe. Iko mifano mingi ya kuthibitisha ukweli huu. Sote tunafahamu kisa cha kijana tajiri aliyemwendea Yesu Kristo akitaka kujua afanye nini apate kuurithi ufalme wa Mungu; na akakutana majibu magumu yafuatayo: "Yesu aliposikia hayo alimwambia, umepungukiwa na neno moja bado; viuze vyote ulivyo navyo vyote, ukawagawie masikini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” (Lk. 18:22)

Maneno haya ya “…viuze vyote ulivyo navyo…” tafsiri yake ni “utoaji wa 100%” kwa kiwango cha Yesu Kristo. Na isitoshe, majibu ya Yesu kwa yule kijana tajiri yalimchanganya Petro akashindwa kujizuia ikabidi amkabili Yesu Kristo kwa swali gumu bila kigugumizi akamuuliza: “Ndipo Petro akajibu akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?” (MT.19:27) Unaona msomaji wangu? Petro anauliza hivi: “…sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?”

Kwa hiyo, mitume na wanafunzi wake Yesu waliacha vyote walivyo kuwa navyo. Hatusomi kwamba waliacha “sehemu ya kumi (10%)” ya vyote walivyokuwa navyo. Waliacha 100% ya vyote walivyokuwa navyo. (Mbeleni katika makala haya nitatafsiri ni jinsi wanafunzi walivyoacha/kutoa vyote yaani 100%)

Turejee kwa majibu ya Yesu kwa Petro yanazidi kufafanua utoaji wa 100% pale aliposema: “Yesu akasema, amin nawaambieni, hakuna aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele.” (MK.10:29-30)

Kwa muktadha wa maandiko haya tunapata kujua kwamba kuacha/kutoa 100% matokeo yake ni "kupata mara mia (100%) ya vile vilivyokwisha kutolewa. Maana yake atapata 100% ya vile alivyoacha au kutoa kwa 100%. Kwa hapa wahubiri wengi tumechukua kipengele cha mwisho tu cha majibu ya Yesu cha “kupokea mara mia” na kuhamasisha watu kutoa lakini hatuwaelimishi sharti ya kiwango cha kutoa 100% kwanza

KWANINI YESU ALIAMURU KUACHA VYOTE (100%)

Jibu la kwanza ni kuwa katika agano jipya Yesu kuanzisha utaratibu wa maisha ya kujikana na kujitoa mhanga kwa ajili yake na kwa ajili ya Injili: “Akawaambia wote, mtu yeyote akitaka kunifuata, ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.” (Lk.9:23)

• Maana ya kujikana mwenyewe

Maana sahihi ya "kujikana mwenyewe" Ishara ya kwanza ya kujikana mwenyewe ni “kuikatalia na kuinyima nafsi yako matakwa yake; na badala yake kuyachukua mapenzi ya Yesu kuwa ndiyo mapenzi yako binafsi."

Ni kuusalimisha uhuru wa utashi wako chini ya mapenzi ya Yesu badala ya matakwa yako binafsi. Ni kumpa Yesu Kristo mamlaka ya juu ya kuwa ndiye mwamuzi wa mwisho kuhusu maisha yako hapa duniani.

Aidha, "kujikana" huku kunakwenda sanjari na “kuwakatalia/kuwanyima/kuwaondolea haki na mamlaka wazazi na ndugu na jamaa wa karibu kushika nafasi ya kwanza ya maamuzi kuhusu maisha yako; na badala yake Yesu Kristo kuwa ndiye nambari moja na mwamuzi wa mwisho wa maisha yako.

Tafsiri ya pili ya "kujikana nafsi" kwa ajili ya Kristo, ni pamoja na "kujivua haki na mamlaka ya kumiliki mali binafsi." Ni kuamua "kuziweka wakfu mali zako chini ya umiliki wa Yesu" ili zitumike kwa ajili yake na Injili, na wewe ubaki kama msimamizi wake lakini si mwamuzi wa mwisho kwa matumizi yake. Ndiyo maana Yesu aliwatia moyo wanafunzi wake kwa kusema: “Bali utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” (Mt.6:33)

• Maana ya kubeba msalaba wako

Muktadha wa kubeba msalaba enzi ya karne ya kwanza haikuwa kuvumilia matatizo ya kimaisha. Tafsiri ya moja kwa moja ya kubeba msalaba ni ishara ya “mateso na kifo cha aibu”! Kwa mantiki hii, Yesu aliposema kila mtu anayetaka kumfuata "abebe msalaba wake kila siku," maana yake, "mtu mwenyewe baada ya kufuata Kristo basi lazima akubali kwa hiari kupatwa na mateso makali, pamoja na kufedheheka sana mpaka kufa pasipo hatia binafsi. Maana yake afuate nyayo za Kristo. Hivyo ndivyo ilivyowatokea mitume na maelfu ya wakristo wa karne ya kwanza, waliteswa na kuabishwa hadi kuuawa kwa ajili ya imani yao kwa Yesu.

Jibu la pili ni kwanini Yesu aliamuru kuacha/kutoa vyote 100% ni kwa sababu hakupenda wanafunzi wake "kutumikia mabwana wawili". Hata wanafunzi wake kumtumikia Mungu na Mali. (Matt.6:24) Kwa mujibu wa Yesu Kristo, kipaumbele cha kutafuta na kujilimbikizia binafsi mali anakitafsiri kuwa ni “utumishi” kamili ambao unachukua nafasi ya kwanza katika moyo, akili, na muda wa mtu kiasi cha kumfanya ashindwe kuyatenda mapenzi ya Mungu. Kumbuka kwamba Amri kuu ya kwanza ni “kumpenda Mungu kwa roho yote, moyo wote, akili zote, nguvu zote. Vitu hivi vikielekezwa katika kutafuta fedha mali tayari vinavutwa huko kuliko mambo ya Mungu na ufalme wake.

JE WAKRISTO WA KWANZA WALIUZA MALI ZOTE NA KUBAKI MIKONO MITUPU?

Hapa sasa ndipo napenda kufafanua ni kwa jinsi gani wanafunzi wa kwanza walivyotekeleza Agizo la kutoa 100% katika agano jipya. Kuna nadharia potofu inayofundisha kwamba wanafunzi wa kwanza waliuza mali zao zote wakabaki hawana kitu chochote. Maandiko hayasemi hivyo hata kidogo.

Ukweli ni kwamba mitume waliwafundisha wakristo wa kwanza kuhusu “kuachilia au kujivua mamlaka ya kumiliki mali kibinafsi” na badala yake Yesu Kristo awe ndiye “mmiliki wa mali zote walizokuwa nazo”; ila tu wao wabaki kuwa ni“mawakili/watunzaji wa mali za Kristo”!

Ushahidi kamili ni katika utekelezaji wa agizo la "kuacha vyote" kama livyonukuliwa hapa: "Na jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu alicho chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika.” (Mdo.4:32)

Maneno ya “wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu alicho chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe” yanathibitisha kwamba wakristo wa kwanza hawakuuza vyote na kubaki mikono mitupu. Walizingatia maelekezo ya mitume wao katika “kuweka wakfu vyote walivyokuwa navyo” viwe mali ya Kristo kama kigezo cha kuwa wanafunzi wa Yesu.

Na hiyo ndiyo tafsiri ya “hapana hata mmoja aliyesema kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe..” Bado waliendelea kutunza mali walizokuwa wanazimiliki tangu mwanzo ila tu kilichobadilika ni "mamlaka ya umiliki kibinafsi". Baada ya kuweka wakfu vyote kwa Yesu, walitambua vitu walivyo navyo si mali yao binafsi, walibaki nazo kama “mawakili/watunzaji wa mali za Kristo”.

Kwa njia hii Roho Mtakatifu aliwaongoza kuuza sehemu ya mali hizo, zikiwemo nyumba na viwanja vya ziada wakawasilisha 100% ya mauzo yake kwa mitume. Na ndiyo maana akina Anania na Safira walikuwa walipoficha sehemu ya mauzo ya kiwanja ambacho walikwisha kukiweka wakfu kuwa mali ya Yesu, na kuahidi kukiuza na kuleta 100% ya mapato yake. (Mdo.5:1-11)

Kwa hiyo, ukweli wa kimaandiko unathibitisha kwamba wakristo wa kwanza pamoja na kutoa vyote kuwa mali ya Kristo; na pamoja na kuuza baadhi ya mali hizo kwa ajili ya kuleta michango kanisani; bado waliendelea kutunza sehemu ya mali nyingine kama nyumba ambazo waliendelea kuzitumia kwa ibada na mijumuiko ya kijamii ambayo ni maslahi ya ufalme wa Mungu.

MATOKEO YA UTOAJI WA 100%

Utoaji wa 100% ulilifanya kanisa la kwanza kufuta umaskini wa kwa kipato kwa waamini wote! Ndiyo maana tunazoma ya kwamba "wala hapakuwepo hata mmoja mwenye mahijtaji...." Uchumi wa kanisa uliinuka kwa kuwa walianzisha vikundi vya uzalishaji kwa mfumo wa vikundi vya ushirika ambapo wasiokuwa na mitaji waliwezeshwa wakawasilisha na kuleta gawio la faida kwenye mfuko mkuu wa kanisa:

“Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni maa mitume; kila mtu agawawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji.” (Mdo.4:34-35)

Historia inasema kwamba, kanisa la Yerusalemu lilikuwa na idadi ya washirika wasiopungua elfu thelathini, na lilidumu kwa miaka 40 na na bado hapakuwepo na mtu hata mmoja aliyekuwa fukara miongoni mwao! Haya ndiyo matokeo ya utoaji wa agano jipya

Asante kwa kufuatilia mfululizo wa makala haya tangu sehemu ya kwanza mpaka hii ya nne na ya mwisho. Najua yatakuwepo maswali mengi na niko tayari kuyajibu kwenye post zijapo kwenye ukurasa huu. Nitakushukuru ukiwarushia marafiki zako wengine ujumbe huu, na pia ili nijue kama tuko pamoja basi nijulishe kwa ku-like post hii. Ubarikiwe sana

Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.