NAMNA YA KUOMBEA NDOTO ZILIZOGUSA MAISHA YAKO (6&7)

Mwalimu Christopher Mwakasege

LENGO LA SOMO NI KUIMARISHA UHUSIANO WAKO NA MUNGU KATIKA KRISTO YESU

>>Kazi ya Mungu ukiifanya kunakuwajibika ndani yake, yaani si kwamba wewe unaeifanya hiyo kazi unastahili sana au uko sahihi sana kuliko wengine hapana bali ni neema yake tu Mungu. Somo hili ni kwa ajili ya kujenga uhusiano wako na Mungu na sio ndoto tu. 

>>Jana nilizungumza na wewe jambo la Tano  la Kuombea Fikra zako zikwamuliwe mahali zilipokishwa au kwama
>>Katika pointi hii ya tano tuliangalia vipengelee kadha wa kadha ngoja nikukumbushe kwa uchache

1 Fikra zinauwezo wa kuetengeneza aina ya maisha na kiwango chake
>>Na tuliangalia Mstari wa Mithali 23:7a

2 Mungu au shetani wanatumia ndoto ili kugusa fikra za mtu
>>Tuliangalia mfano wa Yusufu aliyemlea Yesu na Nebukadreza

3 Ndoto inaweza kutumika kufanya fikra zako kufungwa au kufunguliwa maisha yako
>>Yaani hapa huwa muda mwingine ninapokuja kufundisha huwa nakuja na Karamu yaani kuna vitu Roho Mtakatifu ananiambia hapa ili nikasome na nifuatilie .

4 Ndoto inaweza kutumika kuweka ndani ya Fikra zako umuhimu wa kujua namna ya kujiandaa ipasavyo ili kupata maarifa yanayohitajika katika hatua iliyopo kwa ajili ya maisha yako ya wakati ujao

>>Soma kwa Upya kitabu cha Mwanzo 41:1-46 . Ila mimi nitasoma kwa kuruka ruka Kidogo
>>Kumbuka haya mambo matatu katika hii mistari tutakayoisoma ya Mwanzo 41.
         A) Ndoto (Mwanzo 41:1-7)
         b) Tafsiri (Mwanzo 41:25-31)
         c) Ujumbe (Mwanzo 41: 32-36)

A NDOTO ALIYO OTA FARAO
Mwanzo 41:1-7 Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto. Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu

>>Ukiisoma vizuri hapo utaona hizi ndoto alizoota Farao moja ya ng’ombe nyingine ya masuke. Jitahidi twende pamoja ili tuelewane. Na ukiendela kusoma mistari inayofuata utaona ya kuwa Farao alianza kupata mahangaiko na kuanza kutafuta waganga na wachawi ili wamsaidie kutafsiri ndoto hizi na walishindwa hadi alipoitwa Yusufu.

B TAFSIRI YA NDOTO YA FARAO
_Mwanzo 41:35-31 Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.
Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana_

C UJUMBE WA NDOTO YA FARAO

Mwanzo 41:32-36 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa

>>Na ukienda ndani Zaidi kuanzia Mwanzo 41:39-4 hapa unapata maandalizi ya maisha ya baadae yaani miake 7 ile ya njaa. Baada ya ujumbe ilitakiwa jambo la kufanya, na baada ya kupewa ujumbe tunaona mambo kadhaa  hapa ngoja tuliangalie jambo moja moja.

i) Tafsiri ya ndoto za Farao zilibeba taarifa halisi ya chakula kwa Taifa zima na dunia nzima iliyokuwa inafahamika kwa wakati ule kwa miaka 14

ii) Ujumbe wa Ndoto za Farao zilibeba msisitizo kwa Farao Kutumia vizuri miaka 7 ya shibe ili kujiandaa na miaka 7 ya njaa
  
a). Si kila wakati utapata tafsiri katika ujumbe wa ndoto. Kuna ndoto zinakuja na ujumbe moja kwa moja na ukienda kwenye biblia unaona mistari iko wazi kabisa. Na kuna ndoto zingine zina ujumbe na hazihitaji tafsiri  bali zina ujumbe moja kwa moja. Msisitizo wa ndoto sio tafsiri bali ni ujumbe

>>Haijalishi ndoto imetoka wapi kwa Mungu au Shetani mwenye uhalali wa kutoa Tafsiri ni Roho Mtakatifu , usiende kwa mganga au bali Roho Mtakatifu atakupa cha kufanya juu ya hiyo ndoto hata kama ni ya shetani nayo bado Mungu ndiye atakuambia maana yake nini na ufanye endapo kama shetani anataka kuingilia maisha yako na Mungu ni Mwaminifu atakusaidia.

>>Msisitizo wa leo ni kuwa ndoto inaweza kutokea mara mbili na inaweza isifanane kwenye tafsiri ila inaweza ikawa na ujumbe mmoja, ndio maana Roho Mtakatifu atakusisitiza kufuatilia hiyo  ndoto, na kwa kuwa imetokea  mara mbili ni kuwa wajiandae kwa kuwa Mungu ataitimiza upesi.
>>Na isingekuwa hii mistari na msisitizo wake basi tungejua. Kwa sababu kama Mungu anaweza leta kipindi cha ukame si tunaweza omba kwa Mungu kuwa Baba tunaomba tuepushie hii njaa/huo ukame au aiweke mbali. Lakini inatakiwa tumfahamu Mungu kutoka Kona tofauti tofauti na sio moja tu

>>Ndio maana ukisoma biblia utaona Maserafi katika kiti cha enzi ukisoma katika Kitabu cha Isaya alipokufa mfalme uzia anaposema alimuona Bwana. Maserafi wakawa wanasema utukufu utukufu kwa sababu kila mmoja alikuwa anamuona Mungu kwa namna ambayo hawajawahi kumuona hata siku moja. Na kila mmoja alikuwa anatamani mwenzie aweze kuona alichoona, lakini kila mtu aliona kwa tofauti sana.

>>Hakuna mtu anaweza kumjua Mungu kabisa, bali tunajua kwa sehemu na Mungu kila siku ni mpya na haijalishi nasoma biblia kila siku nimemaliza yote lakini narudia tena kusoma na Napata kitu fresh kabisa na kipya na Zaidi sana ninapokufundisha kuliko ninavyosoma kwa ajili yangu mwenyewe. Mungu kila siku ni mpya.

>> Ili uishi vizuri kipindi kijacho unahitaji kujiandaa au kuandaa maandalizi yake katika kipindi hiki cha sasa kwa sababu maandalizi yanatakiwa katika kipindi hiki cha sasa ili kuweza kuishi katika kipindi kijacho

>> Kama umekuwa ukinisikiliza nimekuwa nasisitiza sana katika kipindi hiki cha uwingi kuwa ndicho kipindi cha kuandaa kwa ajili ya kesho. Ukiona upo kwenye uwingi kuwa makini hiyo ni fursa nzuri sana ya kutengeneza mambo yako yajayo kwa kutumia kipindi hicho.

c) Hekima ya Mungu inahitajika leo ili kuunganisha roho na akili za mtu ili  awe na maarifa ya kujiandaa ipasavyo kwa ajili ya Kesho akiwa kwenye nafasi aliyopo leo
Mwanzo 41:8,33 Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo. Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri

KATIKA MISTARI HII KUNA VITU VINNE NATAKA UONE
1.Roho Kufadhaika
2.Akili
3.Hekima
4.Nafasi/cheo ambacho/ambayo ataitumia kuwa na maamuzi juu ya kipato kwa ajili ya kuweka akiba.

>>Roho ya Mtu bila akili kushiriki si rahisi kuweka akiba leo kwa ajili yake kesho, na hekima ya Mungu inakupa mtazamo wa kuweka akiba sawa sawa na mipango ya Mungu juu ya maisha yao.
Mithali 30:24-25 Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo; Lakini vina akili nyingi sana. Chungu ni watu wasio na nguvu; Lakini hujiwekea chakula wakati wa hari

Mithali 6:6-11 Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno. Ewe mvivu, utalala hata lini? Utaondoka lini katika usingizi wako? Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha

>>Chungu ni wadudu wanaoishi katika nchi za baridi na hujiwekea akiba kabla kipindi cha baridi hakijafika. Na wanayafanya yote haya bila ya kuwa na kiongozi ndio maana biblia inasema hawana akida na hujiendesha wenyewe. Maana yake Mungu anasema hata yeye katupa hii hekima ya kuweza kutunza akiba. Ila sasa Mnyama anaitumia ila ni shida kwa mwanadamu kuitumia hekima hii.

>>Ndio maana biblia inasema ewe mvivu tafakari njia zake/ mikakati yake ili upate hekima yaani andaa maisha ya kesho kwa kutumia leo yako. Maana maisha yanaandaliwa katika kipindi cha shibe na sio njaa na ndio maana hata Silaha huwa inaandaliwa katika kipindi cha Amani na sio kipindi cha vita. Akili zako ziko kwenye nafsi na kazi yake ni kutumia wazo linaloingia kwa ajili ya kuweka akiba ya maisha ya baadae.

>>Uvivu wa kufikiri kwa ajili ya kesho yako biblia inasema umasikini utakujia ghafla kwa sababu hukujua kujipanga mapema. Na ndio maana unaona mtu amekuwa yuko vizuri sana akiwa kazini au akiwa anafanya biashara endapo biashara yake ikiyumba kidogo tu unaona ile taabu anayoipitia na namna Uchumi wake unavyoyumba.  Kukosa akiba ni matokeo ya uvivu wa kufikiria na Mungu kamuweka chungu kwenye maandiko ili akusaidie kuweza kuzungumza na wewe ili ujue unahitaji hekima hii ya kuweka akiba.

d) Muhimu kujali muda wa leo na matumizi yake katika kupata maarifa leo yanayohitajika kujiandaa leo kwa ajili ya kesho

>>Swala la muda na matumizi yake kazungumza kwa kifupi sana ila kwa kirefu Zaidi kazungumzia suala la maarifa yanayohitajika katika kipindi cha shibe kwa ajili ya kipindi njaa.  Nataka nikufundishe kwenye suala la matumizi ya muda wa kuweka akiba, usiweke akiba bila kupiga mahesabu ya muda. Maana akiba itaisha na bado wewe utakuwa na uhitaji.

>>Weka akiba yako kwa muda maalumu yaani akiba yako iendane na muda utakaoihitaji. Kwa mfano kwa habari ya taifa la misri akiba ilihitajika kwa miaka 7 na Mungu aliweka msisitizo sana katika jambo hili na ndio maana alisema na akiba ilindwe (Mwanzo 41:35) Sasa  ile hali ya kuja kuishi kwa miaka 7 ya njaa ilihitaji  sehemu ya tano yaani 20% ya mavuno ya mwaka mmoja. Na hili jambo la mifuko hifadhi ya jamii ya kutunza asilimia 20% ya mshahara wa mtu ilitoka hapa. Wengine hawajui ona. Kuna mfumo miwili ya uchangiaji yaani 10% ya mwajiri na 10% ya mwajiriwa au 15% mwajiri na 5% mwajiriwa. Sasa ukijumlisha unapata 20% haya mambo yametoka kwenye biblia na sheria ya kuweka akiba nayo imetoka kwenye biblia (Mwanzo 41:35) aliposema na chakula kilindwe ina maana akiba nayo ilindwe na ilindwe kivipi ni kwa sheria

>>Ile akiba yao ilihitaji asilimia 20% tu ya mavuno ya mwaka na kuweka kwenye ghala za kitaifa na matumizi yake yangetosha mwaka mzima. Pia maarifa yalihitajika sana kuweza kuweka mambo sawa yaani takwimu kujua ni kweli mavuno yaliyotunzwa yamekuwa 20% kweli au sio na kuhakikisha maghala yamejengwa, kuhakikisha kuna watu wa kusimamia hili jambo pia  kuhakikisha kuna vitu vya kutunza nafaka ili isiharibike. Kwa hiyo halikuwa ni jambo dogo kabisa lilikuwa linahitaji maarifa makubwa sana na hekima ya hali ya juu sana. Kwa sababu pesa ilihitajika kutengwa kwa ajili ya kufanya jambo hili si unajua lazima kama kulikuwa na vikao vilikuwa vya moto sana maana unakuta mna mambo mengi sana. Watu wanasema hatuna dawa, mdawati, elimu, barabara alafu wewe unawaambia kutunza chakula wanaweza sema Mungu mwenyewe anajua, maana najua sio wote walielewa kwa hiyo ndio maana hekima ilihitajika sana, usione ilikuwa kazi rahisi kwa Yusufu ilikuwa ni ngumu sana.


>>Yusufu hakuwa mvivu wa kufikiri na yeye ilibidi afikiri kwa niaba ya taifa zima juu ya kesho yao. Kwa sababu hata wewe hata kama unajiongoza wewe mwenyewe jifunze kufikiria juu ya kesho yako weka mipango yako ya mbele miaka mingi ijayo na anza kuitekeleza mmoja mmoja.  Nilikuwa mkoa mmoja kiongozi mmoja alinijia alisema Mwakasege umenipiga ngumi za uso  nikasema kwanini alisema uliposema. Kiongozi hauruhusiwi kuishi kama watu wengine au kufikiri kama watu wengine, wewe unatakiwa uishi mbele yao yaani wao kabla hawajafika kesho wewe uwe tayari umefika kesho.  Majukumu ya kiongozi sio kuwauliza wananchi wanahitaji nini ina maana ukiwa hivyo hauna haja ya kuwa kiongozi. kiongozi ni lazima uwe na uwezo wa kuona mbele kuliko watu unaowaongoza.

>>Nilikuwa nasoma ushuhuda mmoja wa kijiji Fulani hivi nchini Brazil na viongozi wa pale walipoenda kuwauliza wananchi kuwa wanahitaji nini na wananchi walisema ngoja tufikirie kwanza na baada ya muda kidogo wakasema wanahitaji kiwanja cha mpira. Wakati huo huo walikuwa hawana shule na hospitali. Na ukiwa kama kiongozi unahitaji kujua kuwa hawa watu japo wanahitaji kiwanja cha mpira hawawezi kucheza mpira bila kuwa na Afya. Kwa hiyo unapeleka hospitali kwanza na shule ndipo unapeleka kiwanja cha mpira. Maana huwezi kuwa kiongozi na ukamfurahisha kila mtu, maana wapo tu watakao kuchukia.

>> Watu wa Misri walikuwa wavivu wa kufikiria, kipindi cha shibe kilipoisha walisema hawana chakula, sasa swali ni kuwa walikuwa wapi wakati serikali yao inaweka akiba ya chakula kwani wao walikuwa hawaoni? Njaa imeingia ndipo wanataka mbegu ya kwenda kupanda  maana wao walikuwa na akiba ya pesa na wanyama na zilipoisha biblia inasema Yusufu aliwahamisha akawaweka kwenye matuo kwa sababu alinunua ardhi yao yote. Na hata alipowaweka kwenye matuo nako bado aliwapa mbegu kwa kuwauzia.

Mwanzo 47:14- 26 Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao. Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha. Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha. Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula badala ya farasi, na badala ya kondoo, na badala ya ng'ombe, na badala ya punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule. Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele ya bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu. Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee
Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao. Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu. Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao. Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi. Itakuwa wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakuwa zenu wenyewe, kuwa mbegu za nchi, na chakula chenu, na chakula chao waliomo nyumbani mwenu, na chakula cha watoto wenu. Wakasema, Umetulinda hai, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao. Yusufu akaifanya sheria kwa habari ya nchi ya Misri hata leo, ya kwamba sehemu ya tano iwe mali ya Farao. Ila nchi ya makuhani tu haikuwa mali ya Farao

>>Hii ni habari ya ajabu sana maana Tunaona pia kodi kuanzishwa kwa sababu alisema ‘’ Itakuwa wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano’’ sehemu ya tano maana yake ni asilimia 20 na sehemu ya nne ni 80%  kwa hiyo kodi hapa ndipo ilipozaliwa ilitakiwa watoe 20% ya mapato yao kama kodi. Na ndipo kodi ilipozaliwa.  Yaani walipangiwa hata mfumo wa kuishi wewe soma hiihabari pole pole na Roho Mtakatifu akisaidie kupata cha kuona.

>>Nazungumza na wewe ni kitu gani kinakufanya uwe na akiba kubwa ya mkaa kuliko chakula. Ndiyo una stoo sasa ona una madebe mangapi ya chakula, unaweza sema mimi natunza hela ya kununua chakula si hata wamisri walitunza hela ila sasa ziliwasaidia nini katika kipindi cha njaa? Bado hazikutosha.  Utumie muda vizuri kwa ajili ya kutunza chakula nyumbani kwako.  Na jambo hili lilimlazimu Mungu kuzungumza na mtu katika ndoto na ndio maana unaona watu wengi wanaota ndoto wanarudi shule au wako shule  Mungu anakurudisha tena nyuma ni sawa umemaliza chuo kikuu sawa ila una akili kama za Primary. Na mwingine anarudishwa kazini na Mungu anasema maandalizi hayako vizuri na anasema je ukifukuzwa kazi utaishije? 

>>Au Mungu anazungumza na wewe kwa njia ya ndoto kuwa umefeli mtihani au unapitiliza mlango au uko kazini na wewe unacheza cheza tu Mungu anakuambia kuwa tumia muda vizuri muda wako usicheze cheze na muda.

>>Kuna kijana mmoja nilipokuwa mkoa mmoja alikuja na kusema baba kwa kweli sielewi maana sasa nimeshuka kidogo na maksi zangu zimekwenda chini na sijui nifanyeje maana mara ya kwanza nilikuwa vizuri sana ila sasa nimejaribu hata kuongeza bidi lakini bado nashuka kila siku. Hapo hapo nikuwa namuuliza Roho Mtakatifu kujua shida ni nini aliniambia kuwa shida ni siku moja alinyolewa nywele kwenye ndoto. Nikamuuliza kijana ulinyolewa nywele kwenye ndoto akasema ndiyo nilinyolewa kwenye ndoto alisema ndiyo na mahali aliponyolewa nywele hazijaota mpaka leo. Alikamatwa ufahamu kupitia kwenye nywele zake. Na ndio maana biblia inasema nywele ni utukufu na ndio maana wale wazee huwa wanataka nywele za kwanza za mtoto na huzipeleka kwenye mizimu ha mtoto yule akikua mapepo yanaanza kumfuatilia na huweza hata kumuadhibu endapo atakiuka masharti yao.  Kwa hiyo ukiota ndoto upo kwa kinyozi fikiri mara mbali.

>>Vitu vingine ni vigumu kuelewa ila unakuta tunaposma baadhi ya ndoto huwa tunashangaa maana kuna zingine ziko straightforward na unaona na mstari kwenye biblia lakini unakuta mtu haoni. Muda mwingine unakuta tayari ndoto nimeshaitolea ufafanuzi lakini bado mtu anauliza ina maana hakuelewa nilipokuwa natoa ufafanuzi hapa madhabahuni na unajua tu huyu mtu anahitaji maombi.

MUDA WA SHULE
Daniel 1:1-5 Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, NebukadrezaBwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana
vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao. Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme¬¬

>>Kazi ya shule ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya kesho.  Sasa ile kazi aliyokuwa anahitaji Nebukadreza ilikuwa tayari chini ya wachawi na waganga  na alikuwa bado hajapata watendaji kazi wa kubadili zile nafasi zao. Kwa hiyo ilitakiwa akina Daniel na wenzao waweze kuandaliwa vizuri  kwa ajili ya kuchukua nafasi hizo. Na walipewa maarifa kwa miaka 3 kwa ajili ya kuja kukaa kwenye ikulu ya mfalme.

>>Shule inatoa maarifa yanayohitajika kwa wakati Fulani ndio maana utona kuna kozi ya mwaka 1, miaka 2 au miaka 3 au 5 kwa ajili ya kutoa maarifa maalumu.  Kwa hiyo maandalizi yalihitajika ili kuweza kuwandaa lakini ilitakiwa kwanza wawe na msingi yaani elimu ndiyo maana waliotuandalia mitaala ya elimu walijua kabisa huwezi toka primary alafu uende chuo kikuu, kuna ngazi za elimu inabidi upite kwanza alafu ndipo uweze kwenda chuo kikuu. Ndio maana sekondari ni miaka 4 na high school ni miaka 2 na chuo ni miaka 3 au 4 au 5 au 7 kutegemea na kozi unayosoma. Huu ni wakati wako wa shibe usicheze na muda huo shikilia omba Mungu akusaidie kuutumia vizuri huo muda maana huo ndio utakuja kujenga maisha yako ya baadae na biblia inasema msike sana Elimu usimwache aende zake maana huo ndio uzima wako.

>> Nebukadreza aliwachagua hao watu na akawapa maarifa na Daniel na wenzake walipata nafasi ila sasa wale wenzao maana lazima darasani walikuwa wengi na hawakupata nafasi ya kuchaguliwa kufanya kazi ikulu ya Nebukadreza. Na muda wao ulipotea  na Ile miaka mitatu ya akina Daniel chuo  iliwasaida kwa muda mrefu sana na waliyatumia katika kipindi cha Nebukadreza, Dario na Koreshi. Lakini yalikuwa ni maarifa ya miaka 3 waliyoyapata ndiyo yaliyodumu kwa Zaidi ya vipindi vitatu.

>> Kiongozi Fulani alinipigia na alisema Mwakasege nilikuwa nasikiliza semina yako uliyosema kuwa soma ili kupata maarifa na sio elimu.  Alinisimulia kuwa alikuwa na mwekezaji mmoja hapa nchini na alihitaji watu wa kufanya kazi na sisi tulienda kuongea nae ili aajiri vijana wetu waliomaliza hapa nchini, lakini yeye ataajiri mchanganyiko. Yule mwekezaji alichagua vijana mchanganyiko, wengine form four na wengine form six na wengine chuo kikuu. Basi baada ya mwaka mmoja kuna sehemu aliondoa wa form four akabakiza wa chuo kikuu, na pengine alitoa wa chuo kikuu na akabakiza form six na form four. Basi wale wa chuo kikuu wakaanza kulalamika kuwa kwanini umetuacha sisi, yule mtu alisema neno gumu kidogo MIMI SIAJIRI CHETI, AU ELIMU BALI NAAJIRI UTENDAJI KAZI YAANI MAARIFA

>>Akina Daniel walimkaribisha Mungu katika maandalizi yao na ndio maana aliwasaidia katika kupata kazi, ukiamua kumuweka Mungu katika fahamu zako au akili zako na katika kipindi chako cha maandalizi huwezi kosa kazi. Mungu anakuandaa kwa ajili ya kukupa kazi na uwe na uhakika lazima kazi utapata.  Ndio maana inamlazimu Mungu kukusemsha kwa njia ya ndoto baadhi ya mambo na kukuonesha kuwa uko shuleni na unafanya mtihani na muda mwingine anakuonesha na aina ya mtihani yaani hapo anakuonesha kuwa Fikra zako zimekwama mahali inabidi zinasuliwe

KUNA AINA MBILI ZA MITIHANI

1.Mtihani wa darasani na  kwa ajili ya kupima elimu uliyoipata baada ya masomo uliyosoma
2.Mtihani wa interview (usaili) Kwa ajili ya kupata kazi, ina maana unapima maarifa uliyoyapata baada ya kumaliza elimu. Hii haifanani maana unakuta mtu katoka interview anasema Bwana hawa watu wameuliza swali ambalo hata ambalo sikusoma.  Swala sio kusoma walikuwa wanapima je una maarifa ya kukutosha kufanya ile kazi wanayoihitaji.

MFANO WA DAUDI
>>Daudi alipakwa mafuta mara tatu
     ~~Nyumbani kwa baba yake Yese Samwel alipomfuata Nyumbani kwao
     ~~Alipokuwa Hebroni ili awe mfalme wa Yuda
     ~~ Wazee wa Israel walipompa ufalme wa kuwa Mfalme wa Israel yote

>> Sasa Daudi alitawala Israel kwa muda wa miaka yote 40  lakini miaka 40 inahesabiwa kuanzia pale alipokuwa amaenza kutawala Yuda. Sasa swali ni je katika kipindi cha upako wa kwanza kwanini hakihesabiki?  Ina maana ule upako ulikuwa kwa ajili ya maandalizi.

>>Upako wa Maandalizi ni  kwa ajili ya kumuandaa mtu, hiki ni kipindi muhimu sana kwa mtu maana unaona daktari huyu anakutibu kwa dk tano tu maana anajua wewe una kazi nyingi sana za kujenga taifa na hata hataki kupoteza muda wako lakini yeye ilimchukua miaka 7 kujifunza.   Au yule daktari wa meno ilimchukua miaka 5 kujua kutibu meno na ukapona unaanza kusema “Loli unganga uju nnunu mwee likabhabhapo nu kubhabhapo” Maana yake ni kuwa Huyu daktari ni bingwa/mzuri sana kwa sababu sijapata hata maumimivu) lakini yeye huyo imemgharimu miaka 5 kujua kukutibu.

>>Hivi unajua kitu unachojifunza hapa kwa lisaa limoja mimi nimetumia Zaidi ya masaa 4 -5 hadi sita ili kuandaa na ina maana yale masaa manne au matano kwangu yanakuwa blocked kwa sababu ni ya maandalizi.  Na muda mwingine wananikaribisha kuwa karibu siku moja Kansan kwetu, uje ufundishe ile siku moja ya kujifunza wewe itanichukua siku 3 au nne kujiandaa. Kwa hiyo kuna sehemy siendi si kwa sababu sina somo bali ni kuwa sina muda wa kutosha kujiandaa.

>>Nazungumza na wewe vitu vigumu kidogo tumia vizuri ule muda wa maandalizi na rasilimali zake. Unapopata pesa ina maana hiyo ni miaka ya shibe yaani uwingi tumia vizuri weka akiba fanya hela yako izalishe. Na ukikosa akiba usiende kwa Mungu kutafuta msaada kwanza maana msaada ni mzuri kwa kitambo na ukizidi sana utakulemaza. Kwa hiyo anza na Toba ili Mungu anapokupa msaada akupe na mbegu pia na kuzifanya Fikra zako zifikiri.

Tunaenda kufanya maombi hapa

Unahitaji kutafuta kanda ya leo maana ina vitu vizuri sana na itakusaidia san sana. Hizi summary ni sehemu tu ya kukujulisha kilichokuwa kinaendelea uwanjani. Ukiwezapata pata Kanda hii. Kama uko mbali tembelea www.mwakasege.org  kupata maelezo au kuwasiliana na huduma ya MANA kujua namna ya Kupata Kanda

>>Miaka ile ya 80 wito ulikuwa unawaka sana ndani yangu na nikajua kumtumikia Mungu ni kwenye uimbaji basi nikajiunga na kwaya na mwalimu aliniuliza naimba sauti ya ngapi nikamwambia sauti ya….
 Basi akanipa zoez dogo na kuimba na kwa kweli nadhan hata yeye alishindwa kuniambia ukweli kuwa ile sauti yako sijailewa  kwa sababu sauti ilkuwa inapanda na kushuka mara naimba base mara sauti ndogo basi akasema jaribu sauti ya kwanza. Nikajaribu mara akanihamisha sauti ya nne, nako nikaona sifit kwa sababu niliona kuna watu wabase nzuri kuliko ya kwangu. Basi nikahamaia kwa wapiga vyombo nako niliona wako watalaamu kunishinda. Basi nikaanza kupiga mabati (crash)  na nilitunga hata style yangu ya kupiga.  Na niliota ndoto kuwa napelekwa shule ya kuimba  na ndipo niligundua kuwa nako kuimba kunahitaji kujifunza. Sasa nina nyimbo kadhaa nimetunza ili wasije wakaniibia na ziko kadhaa ntatoa albamu yangu na nikiona haitoshi ntaweka na tenzi kidogo

>>Baada ya hapo yalifanyika maombi sana ya kuombea watu wote wanaopata shida kwenye shule hasa vijana. Na hakika nguvu ya Mungu ilionekana sana pale uwanjani.

>> Ili semina hizi ziwe msaada kwako hakikisha unaokoka na unamjua Mungu kama hujaokoka hakikisha unaokoka maana huu ndio mtaji mkubwa sana. Fanya maamuzi hayo leo na ukishaokoka soma somo la utangulizi kwenye link hapo chini na jiunge na waliokoka walioko kansani kwako.

Siku ya Saba

 >>Najua leo kuna wengine ni siku yao ya kwanza kuja kwenye semina kwa sababu mbali mbali hawakuweza kufika ila jitahidi pata kanda za masomo haya. Na unaponunua kanda hizi usiende na wazo na kununua au iwe ni kitabu au ni nyimbo za watumishi wa Mungu maana huwezi linganisha thamani ya pesa yako na kilichoko ndani. Tunafanya hivi ili kupanua wigo sio kwa ajili ya kupata faida. Kanda hizi ni chakula chukua sikiliza na kusikiliza. Kama uko mbali tembelea www.mwakasege.org utapata maelezo ya namna ya kupata kanda na vitabu. 

SUMMARY YA MAMBO TULIYOJIFUNZA KWENYE SEMINA.

1 Usidharau wala usipuuzie ndoto uliyoota kwa maana ndoto ni lango mojawapo la kiroho
2 Vijue vyanzo vya ndoto na jua namna ya kuviombea ipasavyo.
3  Ng’oa kilichopandikizwa na shetani kupitia ndoto na madhara yake.
4 Kuombea tafsiri ya ndoto kusikuzuie kuombea na ujumbe wa ndoto husika.
5 Ombea Fikra zako zikwamuliwe mahali zilipokwamishwa kupitia ndoto ulizoota.
6.Tumia uhusiano wa neno na Roho Mtakatifu ukusaidie kuombea ndoto ipasavyo.

LEO TUTANGALIA JAMBO LA 6 TUMIA UHUSIANO WA NENO NA ROHO MTAKATIFU UKUSAIDIE KUOMBEA NDOTO IPASAVYO


Yohana 15:7 Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Warumi 8:26-27 Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu

>>Kutumia uhusiano wa neno na Roho Mtakatifu. Kama unataka kuomba vizuri inabidi neno la Mungu likae kwa wingi ndani yako. Na inategemea sana ngazi uliyopo huo mstari wa Yohana 15:7 inabidi uombe tofauti kidogo ili uweze kutembea kwenye mapenzi ya Mungu. Mungu anaweza akakupa kitu unachokitaka lakini kuwa makini sana. Maana wana wa Israel walipewa Nyama na walikondeshwa Roho zao.  Maana hata huku mjini watu wanasema mtoto akililia wembe….., MALIZIA HAPO

>>Kuna wengine wamepewa vitu wanavyovitaka lakini ni nje ya mapenzi ya Mungu kwa lugha ya kiingereza tungesema kuna Perfect will of God na Permissive will of God. Yaani hii Permissive will of God ni kwa kuruhusiwa na Mungu lakini sio mapenzi ya Mungu. Na wa perfect will of God na huyu wa Permissive will of God hawawezi kuwa sawa hata kidogo.

>> Na nakumbuka mwaka Fulani tukiwa tunaandaa semina ya Dodoma. Na tulikuwa tunaomba Mungu Fanya hiki fanya hiki na Mungu anafanya. Na wakati ule tulikuwa hatuna mahema kama hivi tulikuwa tunafanya semina ndani ya kanisa. Basi tuliwaambia wenzetu wafanye maombi sana juu ya semina ile na walifunga na kuomba kwa ajili ya semina kwa miez kadhaa na kila ijumaa walikuwa wanafanya mkesha wa maombi. Basi na mimi na Mke wangu tuliwahi kwenda Dodoma ili tungane nao kwenye mkesha. Basi tuliomba sana na wenzetu walijitahidi kwa kweli. Sasa iliwadia siku ya Semina hiyo siku ilikuwa ngumu kweli maana nilikuwa naonekana kama naongea peke yangu alafu najiuliza kama watu wamenielewa kweli nikawa naongea alafu naona neno lile kama linanirudia mwenyewe. Ilikuwa ngumu kweli kweli basi nikaita watu kuokoka na walitoka, nilijua hawatatoka kwa sababu sikuwa na uhakika kama wamenielewa.

>>Baada ya pale nikamwambia mke wangu kuwa kwa kweli mimi siombi tena, maana haiwezekani tuombe kiasi kile na kufunga kwa siku zote vile alafu semina iwe ngumu vile yaani kama niko peke yangu maana hata ule uwepo wa Bwana haupo. Basi moyo wangu uliumia sana na nilisema mimi siombi tena siku iliyofuata mke wangu aliniamsha twende kuomba nilimuombia mimi siendi ila nilisema nitakusindikiza tu  basi tulipofika Kansan asubuh akafungua mlango akashuka ndani ya gari na alienda Kansan. Mimi nikavuta kiti ndani ya gari nikaka. Sikuenda kuomba, basi mke wangu alirudi tulirudi pale mahali tulipofikia. Na mchana niliomba chakula nikala na sikufunga tena. Zilipobaki dakika kidogo kabla ya kwenda semina nilimwambia Bwana Yesu unakitu cha kuzungumza na watu wako akanipa na niliandika. Siku ile ilishuka nguvu kubwa sana ya Mungu pale katika semina.

>>Ilipofika jion nilipomaliza semina nilishangaa sana maana sikuomba lakini nguvu iliyoshuka pale ilikuwa ni kubwa sana. Nikamuuliza Mungu sasa ndio nini Mungu alisema neno lango katika Yohana 12:26 Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu na alisema kuwa nikikutuma kufanya semina inabidi uje kwangu kuomba au kuuliza kuwa mimi Mungu ninataka kufanya nini kwenye hii semina, na sio ambavyo wewe unataka kwenye hii semina.

>>Biblia inasema pale nilipo ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa na sio sisi tulipo na Mungu atakuwa. Kuwa makini hapo biblia haijipingi maana mwingine atasema Mathayo 18:20 Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao . Sasa hukusanyiki wewe upendavyo maana ile kazi ya kufundisha au kuhubiri ni lazima Mungu awe amekutuma na kasema  biblia iko wazi kabisa Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo Pale alipo Yesu ndipo utakuwa kumtumikia . Ina maana mwenye kukualika kutumika ni Mungu na inabidi ufanye vile yeye apendavyo maana biblia inasema Mathayo 7:21 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Kwa hiyo ile kusema mnasema Bwana Bwana na mjisahau kuwa mnafanya mapenzi ya Mungu si kweli. Kwa hiyo usipende kumpangia Mungu mambo ya kufanya bali yeye ndiye akupangie wewe maana yeye ndiye mwenye kazi. (Haya maelezo mwalimu hakuongea na hakuweka mistari hii nimeweka baada ya kupata msisitizo ndani yangu kwa ajili ya kutoa ufafanuzi nilipokuwa naandika)

>> Na ndio maana nilikupa tahadhari mapema katika   Yohana 15:7 Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Nilisema usiombe lolote bali omba kulingana na mapenzi ya Mungu Na Biblia hiyo hiyo imesema Yakobo 4:3 Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. _ Na 1 Yohana 5:14-15 Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.

>> Hata Ibrahimu aliomba kuwa Ishmael abarikiwe na ni kweli alibarikiwa nje ya agano, na si watu wengi wanajua tofauti ya kati ya Baraka za agano na Baraka zilizo nje ya agano. Ishmael hakupewa ardhi bali Isaka alipata ardhi. Hivyo ukiota ndoto na usikimbilie tu kuomba bali tafuta uhusiano kati ya neno na Roho Mtakatifu ili upate msaada.

>>Neno na Roho vinafanya kazi kwa pamoja na neno bila Roho Mtakatifu halina msaada kwa sababu katika uumbaji wa Mungu Roho alitulia juu ya maji na Mungu alipokuwa anasema na kuwe Nuru ndipo Roho alikuwa anenda kutenda. Angalia Mwanzo 1:2-3 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru  Lakini ukiangalia kwa habari za kuzaliwa kwa Yesu biblia inasema kuwa neno alitangulia na Roho akafuata. Angalia  Luka 1:30-35 Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu

>>Hapa unaona neno kutangulia yaani kuwa atapata Mimba na ona Mariam alipouliza itakuje ndipo Malaika alisema ‘’ Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli  kwa hiyo neno + Roho Mtakatifu =Matokeo.  Kwa maana Roho Mtakatifu na neno wanafanya kazi pamoja sasa watu wengi hata hawajui kwanini wanakuwa wazito kusoma biblia sasa sijui wanaombaje kwa sababu kuwa na nguvu za Mungu bila neno ni sawa sawa na gari lina kila kitu lakini halina taa maana neno la Mungu ni taa.

>> Na unajua kwanini huwezi kusoma biblia ni kwa sababu hujapangia muda. Kitu ambacho hakina thamani kwako huoni umuhimu wa kukipangia muda. Maana natamani sana watu wawe kama watu wa Beroya wakichunguza chunguza maandiko maana natamani na wao wafuatilie kwenye biblia.

>>Ivi umewahi jiuliza kwanini Yesu aingie gharama ya katukalisha hapa kwenye hema anataka tukae kama darasa ili tujifunze neno na Mungu.  Lakini sasa unakuta mtu haji kwa mkao wa kujifunza bali anasubiri saa ngapi aombewe. Lakini ujue hapa ni semina sio mkutano kwa hiyo kaa mkao wa kujifunza.

>>Je sasa ukifika mahali pa kisiwa cha Patmo utafanyaje maana utakuwa peke yako na sasa utamtafuta nani maana hata simu unakuta hauna ya kuwapigia wapendwa. Sasa Unaweza kusoma biblia kila mwaka maana kuna vitabu vya kuongoza mwongozo wa kusoma biblia kwa mwaka mzima au kwenye simu yako kuna application za kukuongoza namna ya kusoma biblia kwa mwaka mzima. Sasa jiulize ni muda gani unakaa whatsapp au sehemu nyingine na ni muda gani unasoma neno la Bwana, hata kwenye simu yako unaweza weka biblia yako na ukaisoma kila siku.

>> Mungu alisema na mimi katika ndoto nyingi sana.  Nilipokuwa Form Six katika Sekondary ya Mkwawa na sikuelewa maana yake ni nini. Niliota ndoto nikiwa mwisho wa Dunia na watu waliokuwa wanapona ndio waliokuwa wanapita kwenye nyumba niliyokuwamo. Hapo ndipo nilipojua kuwa nimepewa kazi ya kutangaza habari za Mwisho wa Dunia.

>>Pia nikiwa SUA wakati ule ni sehemu ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.  Niliota ndoto mtu mmoja mrefu amakuja na nguo nyeupe na amekuja na kitu cheupe cha Duara na ilikuwa na kishikizo,na mara alisema duniani mna dhambi nyingi mara akaondoka nacho . na Kwa kweli hii ndoto nilishindwa kuvumilia ilibidi niende kwa mganga na rafiki yangu na pikipiki. Na Mganga kidogo apatie tu na nilipomsimulia ile ndoto alisema alisema kweli aliyekuja ni Malaika  na kuna Baraka anataka akupe sasa tatizo sio duniani  kuna dhambi bali ni wewe unadhambi nyingi sana. Na nilimuuliza sasa ndio natubu vipi alinipa utaratibu wa dini ya kwao namna wanavyofanya aliniandikia na ile sala ya toba na akaniambia niikariri. Sasa nilipokuja kuokoka ndipo nilielewa kuwa lile jiwe jeupe lilikuwa ni nini Ufunuo 2:17 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea

>> Nazungumza na wewe umuhimu wa kuweza kutazama uhusiano wako na Yesu na utumishi na maana ni muhimu sana kujua kuwa si kila nguvu ni za Mungu na si kila mtu anayekujia kwenye ndoto amevaa vazi jeupe ni malaika maana hata shetani nae hujifanya malaika wa Nuru.  2 Wakorintho 11:14 Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.

>>Nakuambia vitu vya muhimu na vya kukusaidia ukiona ndoto inakupeleka mbali au inakuondoa karibu na Yesu wako cheki vizuri. Maana si vyote vya kuamini bali fuatilia maandiko.

NDOTO NYINGINE
>> Niliota ndoto nyingine kuna kanisa moja lipo kwenye kijiji Fulani na katikati yake kuna migomba  na niliona kuna mchungaji mmoja na kaingia kila akihubiri katika lile kanisa watu wanakufa, na akihubiri tena theluthi nyingine wanakufa na baada ya hapo akatoka. Na akavua joho basi mimi nikaingia nikasema kwa jina la Yesu amka, nikaamka na wakaamka na nikasema kwa jina la Yesu waliamka tena. Na hadi waliamka wote na hapo ndipo wito wangu nilijua ni kwa ajili ya kanisa yaani kulifufua kanisa la Mungu.

NDOTO NYINGINE
>> Niliota nipo kwenye Bustani moja na ghafla nikamuona Yesu amenitokea na kaja na taji  na ghalfa akaja kwenye benchi nililokaa na ghafla akanichukua juu na akienda juu na mimi nikawa naenda juu sasa na tazama nguo kubwa  nyeupe ikanishukia na ikanifunika hadi chini. Basi nilipofika nikamkuta mke wangu yupo kwenye uwanja na watu wengi sana uwanjani na anasema tulikuwa tunakusubiri. 

>> Na nilipokuja kusoma kwenye biblia kuwa ndipo nilielewa iliposema Luka 24:49 Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata mvikwe uwezo utokao juu na nilijua mke wangu ndiye mwenye uwezo wa kuwakusanya watu na nilianza kumuombea kwa namna ya tofauti sana. Na hadi leo yeye ndiye mratibu wangu mkuu wa wa semina zote.

>>Kwa hiyo unapopata ndoto nenda kwa Mungu yaani jizoeze kuomba tafsiri kwa Mungu ili akupe maana ya hizo ndoto kama Daniel alivyofanya.  Daniel 2:16-17 Basi Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile. Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake
>>Usifanye kosa kama la Yusufu la kuwasimulia ndugu zake maana si wote watafurahia hiyo ndoto yako   bali nenda kwa Mungu ili akupe cha kufanya kama walivyoambiwa akina Daniel na wenzake. 

MFANO
Kuna dada mmoja nilipokuwa mkoa mmoja akasema baba naomba nisaidie. Kuna mwanaume mmoja alitaka kunioa na yeye anamke tayari ya Yeye na alisema kwa mujibu wa dini ya kwao wanaruhisiwa kuona wanawake wengi. Na yule dada aliniambia kuwa yeye alimkataa na alimuambia kuwa yeye kaokoka. Basi yule mwanaume alianza kumuingilia kwa njia ya ndoto. Nilimuuliza unapolala huwa unaomba alisema ndiyo naomba sasa tena najifunika kwa damu ya Yesu.  Basi nikasema ngoja na mimi niombe niliomba kwa njia hizi tano

1. Niliomba kwa damu ya Yesu kutenganisha muunganiko wa kipepo kati ya lango la ndoto na viungo vya uzazi vya yule msichana.
2. Nilikemea lile pepo lililokuwa linakuja na ile sura ya mtu kwa ajili ya kumtesa Yule msichana.
3. Uponyaji kwa ajili ya madhara yaliyompata yule msichana.
4. Kufanga milango na kuzuia asioteshe tena zile ndoto
5. Ulinzi wa Damu ya Yesu ili aolewe na atakapoolewa aolewe vizuri kwa muda wa Mungu utakapofika.

>>Na baada ya muda alikuja kuniambia kuwa baba ile hali haijajitokeza tena. Na ila aliniuliza swali kuwa je wewe ndiyo umeombaje maana na mimi nimeomba kwa damu ya Yesu hiyo hiyo na sijapata majibu sasa wewe ndiyo umeombaje. Nilimuambia shida hapa msichana ni Imani yaani sio kwamba umeokoka basi damu ya Yesu inaweza kufanya kazi bali bali kuwa na imani yaani kuwa na uhakika wa kile unachokitarajia katika imani yako. 

>>Kuna mtu mmoja pia aliniambia kuwa Mwakasege ninaota ndoto nazini na wanyama, ni kweli nilielewa kuwa kuna agano lipo na Pia mwingine aliniambia kuwa aliota ndoto nyoka kapita katika tumbo lake  nilijua kuwa kizazi chake kilikabidhiwa kwa miungu mingine.  Maana yake usiposhughulika na ndoto hizi mara baada ya muda utakuwa unapata wachumba na bila sababu za msingi unakuta wanakuacha.  Na wengine wanaota wanazini na majini hata hawajui maana yake nini  Mambo ya Walawi  17:7 Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi

TAFSIRI YAKE
Usherati wa Kiroho ni Mbaya sana maana ukiachia hivi mara utajiona una mimba na mara unanyonyesha watoto na hali yako inaanza kuwa mbaya sana. Kwa hiyo Damu ya Yesu inaweza pangua kabisa hivyo vitu  na kukufanya kuwa safi .

>>Pia mtu mmoja aliniambia kuwa aliota mbwa kalala kwenye kiatanda chake na mwingine aliota kwenye kitanda chake yeye ni mwanaume wako watatu  yaani yeye na mke wake na mwanaume mwingine. Mwingine pia aliniambia kuwa kaota ndoto kuwa Wanawake wawili wamelala kwenye kitanda pamoja na mume wake   na hakujua cha kufanya.

>>Kwa hiyo ni muhimu sana kujua namna Damu ya Yesu inavyofanya kazi fuatilia somo hili la Damu ya Yesu katika tovuti pamoja na kwenye Ukurusa wa Facebook wa Mwalimu.  Na ukilijua hili neno utakuwa umepata kitu kikubwa sana. Maana Shetani anafurahia sana watu wasijue neno la Mungu.

>> Zoezi shika kidole chako cha ndoa na Mwalimu aliomba sana kuhusu mapepo yaliyokamata vidole vya ndoa na hakika nguvu ya Mungu ilishuka kwa nguvu kubwa sana sana na kutufungua . Na Mwalimu aliachilia sana Baraka kwa watu wote walikuwepo kwenye semina. Hata wewe huko huko Pokea Baraka za Mungu. Na Ubarikiwe sana sana na tuzidi kumshukuru sana Mungu kwa huduma ya MANA na watenda kazi wote  Mungu awabariki sana. Hebu tamka neno la Baraka kwa Hawa watu maana wanajitoa sana sana.  Hadi mafundisho haya tunayapata bure kabisa… ni neema sana sana kwa Mungu basi tuituime vizuri sana.

li semina hizi ziwe msaada kwako hakikisha unaokoka na unamjua Mungu kama hujaokoka hakikisha unaokoka maana huu ndio mtaji mkubwa sana. Fanya maamuzi hayo leo na ukishaokoka soma somo la utangulizi kwenye link hapo chini na jiunge na waliokoka walioko kansani kwako.

Kusoma/Kufuatilia Zaidi Mafundisho ya Mwl Mwakasege tembelea

FACEBOOK
https://www.facebook.com/Christopher-Diana-MwakasegeMana-Ministry-132462780111984/
Youtube
https://www.youtube.com/channel/UC4p4lrpgpNd-9bHPgHJ4xWw

Ustream
http://www.ustream.tv/channel/mwakasegemanaministry

 website
www.mwakasege.org

 na kama umeokoka kupitia mafundisho haya soma somo la Utangulizi katika link hii http://www.mwakasege.org/mafundisho/hongera/utangulizi.htm   

Glory to God Glory to God.

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.