UJUMBE: KUSHINDWA PAMBANO SI KUSHINDWA VITA

Askofu Sylvester Gamanywa
WAPO Mission International.

Mnara wa mashujaa wa vita vya Kagera. ©SeeTheAfrica
Kushindwa katika pambano sio lazima ndio kushindwa vita! Wakati wa vita majeshi yanayopigana hufanya mapambano mengi tena ya aina tofauti! Kila upande hushinda au kushindwa katika baadhi ya mapambano husika. Lakini kushinda vita ni pale ambapo mkakati wa jeshi wa jeshi husika umefanikiwa kulidhoofisha jeshi pinzani mpaka kusalimu amri

Nikikumbukia uzoefu wangu wa vita vya Kagera ambapo tulimpiga Nduli Idd Amin wa Uganda na kulidhoofisha jeshi lake lote! Vita hivi havikupiganwa ana kwa ana kwa wakati mmoja. Yalikuwepo mapambano mengi na mazito! Kila pambano lilifanyika kwa wakati wake na kukoma kwa muda wa masaa au siku kadhaa. Kwa taarifa yako tu, kuna mapambano ambayo tulipigwa na kushindwa vibaya tukarudi nyuma na kujipanga upya! Katika mapambano hayo tuliyopigwa askari wetu walikufa na wengine kupata vilema vya maisha! Pamoja na kushindwa katika baadhi ya mapambano vitani huko hakukuwa ndio kushindwa kwa mkakati wa kivita wa jeshi letu.

Na pia hatukushinda vita vile kwa sababu tulikuwa na silaha kali zaidi! Tulishinda vita vile kwa sababu ya aina ya mkakati wa kivita tuliokuwa nao! Mkakati huo ulituwezesha kulidhoofisha jeshi la Amini kiasi cha kuteka ghala zake za silaha na kulipiga kwa kutumia silaha zake mwenyewe!

MAISHA YA IMANI KATIKA KRISTO NI VITA

Sasa turejee kwenye kiini cha ujumbe huu. Maisha ya imani katika Kristo ni VITA. Narudia kusisitiza tena. Maisha ya imani ni VITA. Na vita hivi huanza tangu siku ya kutubu na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi binafsi.

Ni mawazo potofu pale tunapotafsiri “maisha ya imani” kuwa ni “starehe na anasa” hapa duniani. Yesu Kristo mwenyewe aliweka bayana akisema: “Hayo nimewaambia mpate amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.” (YH.16:33) Hili neno “dhiki” kwa kiyunani ni “thlip’-sis” likiwa na maana ya (i) “kuugulia maumivu ya kimwili au kiakili (anguish)”; (ii) “kutendwa isivyo halali na ukatili (persecution)”; (iii) “matatizo yenye kuhuzunisha, adha (tribulation)”

Unaweza kujiuliza ni kwanini Yesu aliwatabiria wanafunzi wake kupatwa na dhiki ulimwenguni? Yesu mwenyewe anajibu akisema: “Lakini mtachukiwa na watu wote kwa ajili yangu.” (Luk.21:17) Unaona? Yesu anasema “tutachukiwa na watu wote kwa ajili yake.”! Utajiuliza tena ni kwanini tunachukiwa na ulimwengu huu kwa ajili ya Yesu? Yesu mwenyewe anajibu: “Kama mgekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.” (YH.15:19)

VITA VYA KIROHO VINA MAPAMBANO YAKE

Kama ilivyo kawaida ya vita vya kibinadamu; hali kadhalika na vita vya kiroho navyo vina "mapambano" yake! Mapambano haya ni ya kiroho ambayo ni majaribu na mapito na mashambulizi kutoka kwa Ibilisi na mawakala wake!

Unaweza kupitia mapito fulani magumu; au kupatwa na mashambulizi ya kiroho katika eneo la uchumi, afya, mahusiano katika ndoa, changamoto za malezi ya watoto nk. Pengine umejikuta katika mazingira ambayo umepambana dhidi ya jaribu umeishiwa na nguvu za imani; na hata pengine umeshindwa na adui katika pambano hilo. Na sasa uko katika hali ya majuto ukidhani ndio umeshindwa vita vya kiroho. Napenda kukufariji na kukutia moyo. Shetani asikudanganye. Kushindwa pambano sio kushindwa vita.

Katika ulimwengu wa roho bado unazo fursa za kiimani za kuendelea na vita vya kiroho. Simama tena. Fanya toba kwa pambano uliloshindwa. Damu ya Yesu ipo kwa ajili ya utakaso katika hilo na kuanza upya. Mwombe Yesu Kristo akujaze Roho Mtakatifu akupe nguvu za kupambana tena. Yesu ni mwaminifu aliyeahidi kwamba ameushinda ulimwengu. Sisi nasi tunashinda na zaidi ya kushinda kwa ajili yake aliyetupenda.

“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki.” (1 Yoh.2:1)

Ujumbe huu ni kwa ajili ya kila mwamini ambaye amejikuta katika kukata tamaa ya kiroho kwa sababu tu ameshindwa katika pambano fulani; au pengine amekwama katika jaribu na kuanguka dhambini; na shetani anamhubiria kwa ameachwa na Mungu. Wako wengi ambao kwa nje wanaonekana wako vizuri lakini kiroho maisha yao ndani yako mashakani. Haya basi, hata kama wewe si mlengwa katika ujumbe huu, tafadhali usiache kuwarushia marafiki zako wengine maana kila mtu binafsi anapitia mapambano ya vita vya kiroho. Mimi napitia na wewe unapitia. Sote tunapitia katika mapambano ya kiroho. Ubarikiwe sana!

Share on Google Plus

About Elie Chansa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.